Wanahabari wapewa siri ya kuwawezesha kuhoji
28 September 2023, 12:49 am
Kupitia matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 mwanahabari unaweza kuhoji ili kuisaidia jamii
Na Edward Lucas
Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi, Spika msaafu Mhe.Anna Makinda amewaasa waandishi wa habari kuhakikisha kuwa wanasoma taarifa ya Sensa ili kujijengea uwezo wa kuhoji mipango na mikakati mbalimbali
Mhe. Makinda ametoa ujumbe huo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi 2022 yaliyofanyika mwanzo mwa wiki hii Jijini Mwanza
Amesema kupitia matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya 2022 inaweza kumpa mwandishi wa habari mwanga wa kuuliza masuala ambayo hayajafanyika katika jamii na kwamba huwezi kuhoji ikiwa wewe mwenyewe hujui
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema kuwa thamani ya fedha iliyotumika katika Sensa itaonekana endapo matokeo yatatumika kama ilivyokusudiwa.
Awali akizungumzia mafunzo hayo, Mwakilishi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali ambaye ni Meneja wa Takwimu mkoa wa Mwanza, Goodluck Lyimo amesema hii ni awamu ya tatu ya utekelezaji wa Sensa ya watu na makazi iliyohusisha waandishi wa habari takribani 80 kutoka mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera
Amesema lengo la mafunzo ni kuviwezesha vyombo vya habari kuwa na uelewa mpana wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ili viweze kutimiza wajibu wao.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalihusu mbinu za kiuandishi katika uchambuzi wa takwimu kwa ajili ya habari na usambazaji wa matokeo ya sensa yaliongozwa na mada mbalimbali ikiwemo kuijua ofisi ya taifa ya takwimu NBS pamoja na kufahamu wajibu na mamlaka ya kisheria ya namna NBS inavyotekeleza majukumu yake.