Mazingira FM

Mtoto wa miaka 15 akutwa amejinyonga Bunda

28 February 2026, 17:37

Mtoto huyo alitoka ndani ya nyumbani anakoishi na mama yake mdogo na
kwenda kutekeleza tukio hilo la kujinyonga kwenye mti uliopo pembeni mwa nyumba yao.

Na Adelinus Banenwa

Mtoto aliyetambulika kwa jina la Joshua Judicate Muro mwenye umri wa miaka 15, mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyaburundu, amefariki dunia kwa kujinyonga katika kijiji cha Nyaburundu kata ya Ketare halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara

Akizungumza na Mazingira FM, Mwenyekiti wa kijiji hicho Hamisi Said Madoro amesema tukio hilo limetokea leo tarehe 27 Februari 2026 majira ya asubuhi, ambapo mtoto huyo alitoka ndani ya nyumbani anakoishi na mama yake mdogo na kwenda kutekeleza tukio hilo la kujinyonga kwenye mti uliopo pembeni mwa nyumba yao kwa kutumia kamba ya manira.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, amesema marehemu aliacha barua akieleza kuwa “tangu kufariki kwa baba yake alikuwa akihisi mambo hayaendi sawa na kuamua kujinyonga, huku akimshukuru mama yake mdogo”

Inaelezwa na mwenyekiti kuwa tangu tarehe 24 Februari 2026 mtoto huyo alikuwa akiulizia kuhusu baba yake, akionesha hali ya huzuni kufuatia kifo chake.

Jeshi la Polisi limefika eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi, na baada ya kukamilika kwa vipimo vya awali, mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Sauti ya Mwenyekiti wa kijiji hicho Hamisi Said Madoro