Mazingira FM
Mazingira FM
6 January 2026, 9:09 pm

Msaki amesema katika zoezi hilo wanakumbana na changamoto kadhaa ikiwemo watu kutaja makaburi ambapo ukichimba unakuta hamna kitu hivyo kuwepo kwa makaburi hewa.
Na Adelinus Banenwa
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara imeanza zoezi la uhamishaji wa makaburi ili kupisha ujenzi wa mradi wa njia ya umeme wa Bunda – Ukerewe.
Magreth Nyambwa ambaye Afisa afya halmashauri ya wilaya ya Bunda amesema katika zoezi hilo wanatarajia kuhamisha jumla ya makaburi 61 ambayo yapo kwenye vijiji 11 kwa halmashauri ya wilaya ya Bunda ambavyo ni , Bulendabufye, Bulamba, Chitengule, Igundu, Kisorya, Mahyoro, Makwa, Masaunga, Mwibara, Namibu na Nampangala.
Magreth amesema zoezi hilo limeanza tangu tarehe 15 Dec 2025 kwa kupita nakutambua makaburi hayo kisha leo Jan 6 zoezi la uamishaji linaendelea ambapo kwa siku ya kwanza tayari vijiji vinne vimefikiwa kati ya vijiji 11.

Nasri Msaki mpima Ardhi kutoka shirika la umeme Tanzania TANESCO amesema umeme huo utakuwa wa Msongo wa Kilovoti 132 kutoka Gridi ya taifa na njia hiyo kutoka bunda hadi ukerewe una urefu wa Kilometa 98 na upana wa njia hiyo utakuwa ni mita 27 ambapo wananchi wote waliopitiwa na mradi huo 1298 na kati ya hao wananchi 1179 tayari wamelipwa fidia zao na wachache waliobaki ni kwasababu mbalimbali.
Msaki amesema katika zoezi hilo wanakumbana na changamoto kadhaa ikiwemo watu kutaja makaburi ambapo ukichimba unakuta hamna kitu hivyo kuwepo kwa makaburi hewa pia changamoto ya baadhi ya ndugu kudai hawana sehemu ya kwenda kuwahifadhi ndugu zao kutokana na maeneo yao yote kuchukuliwa katika mradi huo.

Kwa upande wao baadhi ya ndugu waliokuwa wanahamisha miili ya ndugu zao wamesema wameridhishwa na zoezi lilivyoendeshwa kwa kuwa wameshirikishwa kila hatua.