Mazingira FM
Mazingira FM
6 January 2026, 10:59 am

Taarifa iliyotolewa kwa njia ya simu na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Augustin Magere, chanzo cha moto huo kimebainika kuwa ni sebuleni mwa nyumba hiyo.
Na Thomas Masalu,
Majanga yameikumba familia moja katika eneo la Nyarusurya, Manispaa ya Musoma mkoani Mara, baada ya watu watatu kupoteza maisha yao kufuatia moto mkubwa ulioteketeza nyumba waliyokuwa wamelala usiku wa kuamkia leo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa njia ya simu na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Augustin Magere, chanzo cha moto huo kimebainika kuwa ni sebuleni mwa nyumba hiyo kabla ya kusambaa kwa kasi na kuunguza vyumba vinne vya makazi, hali iliyosababisha vifo vya watu hao watatu.
Kamanda Magere amewataja waliofariki kuwa ni Rochi Shaban (39), baba wa familia na mmiliki wa nyumba hiyo ambaye pia alikuwa Meneja wa Ubora wa Maji Mkoa wa Mara, mke wake Mariam George Msigwa (34), pamoja na mtoto wao Rouch Mkole (4).
Katika hatua nyingine, Kamanda Magere amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuwa waangalifu wanapotumia vifaa vya umeme na moto majumbani, hususan nyakati za usiku, ili kuepuka matukio kama hayo yanayosababisha hasara za maisha na mali.