Mazingira FM

Mtoto wa miaka 3 anusurika kifo kwa mateso ya shangazi

11 December 2025, 10:48 am

Afisa utawi wa jamii kata ya Kisorya Edphonce Luben

Mbali na kipigo alichokuwa akipigwa mtoto huyo pia alikuwa akifanyishwa kazi zilizokuwa juu ya uwezo wake kama vile kuosha vyombo, kufagia nyumba na wakati mwingine alikuwa akinyimwa chakula kabisa.

Na Adelinus Banenwa

Mtoto wa miaka 3 jinsia ya kike jina limehifadhiwa mkazi wa kata ya Kisorya kijiji cha Masaunga anaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha afya kata ya Kisorya halmashauri ya wilaya ya Bunda kutokana na kipigo alichokuwa akikipata kutoka kwa shangazi yake aliyekuwa anaishi naye.

Akizungumza na radio Mazingira fm afisa utawi wa jamii kata ya Kisorya Edphonce Luben amesema taarifa za mtoto huyo kufanyiwa ukatili walizipata kutoka kwa mwenyekiti wa kijiji na walipofika ni kweli walimkuta mtoto huyo ana hali mbaya kwa kuwa mwili wake wote ulikuwa umejaa vidonda kutokana na kipigo na zaidi alikuwa na kidonda kikubwa usoni kilichodaiwa shangazi yake huyo alimpiga.

Edphonce ameongeza kuwa mbali na kipigo alichokuwa akipigwa mtoto huyo pia alikuwa akifanyishwa kazi zilizokuwa juu ya uwezo wake kama vile kuosha vyombo, kufagia nyumba na wakati mwingine alikuwa akinyimwa chakula kabisa.

Edpphonce amesema baada ya kukuta hali hiyo walimchukua mtoto na kumpeleka kituo cha afya kisorya kwa ajili ya matibabu na mlezi wake huyo amekamatwa na jeshi la polisi ambapo atafikishwa mahakamani kutokana ana ukatili aliyoufanya.

Sauti ya afisa utawi wa jamii kata ya Kisorya Edphonce Luben
Afisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Bunda anayeshughulikia masuala ya watoto Liberates Mashirima

Naye afisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Bunda anayeshughulikia masuala ya watoto Liberates Mashirima amesema kuwa wananchi wanalo jukumu la kutoa taarifa za ukatili zinazotokea kwenye maeneo yao ili kutokomeza kabisa mambo hayo kwenye jamii.

Amesema halmashauri ya wilaya ya Bunda kupitia elimu zinazotolewa hali ya ukatili mwaka huu imepungua ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo kwa mwaka huu hali imeshuka hadi asilimia 30 ukilinganisha na asilimia 52 ya mwaka 2024.
Liberates ameongeza kuwa wanapopata taarifa na kweli mtoto akithibitisha kwamba fulani ndiye aliyemfanyia ukatili basi kesi hiyo inakwenda mahakamani na mahakimu pamoja na jeshi la polisi wamekuwa msaada katika kusaidia kesi hizo.

Sauti ya afisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Bunda anayeshughulikia masuala ya watoto Liberates Mashirima