Mazingira FM
Mazingira FM
18 November 2025, 9:06 pm

Umekuwa ni utaratibu wa Bank hiyo kutenga asilimia moja ya faida yao kwa mwaka kuirejesha katika kusaidia jamii katika huduma mbalimbali za kijamii kama vile afya na elimu.
Na Adelinus Banenwa
Imeelezwa kuwa umbali kutoka nyumbani hadi shule ilikuwa ikipelekea wanafunzi wengi kuacha shule katika kijiji cha Manchimweru kilichopo kata ya Mugeta Halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Hayo yameelezwa na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Manchimweru wakati wa kupokea msaada wa madawati kutoka Bank ya CRDB ambapo wamesema kabla ya kujengewa shule hiyo walikuwa wanatembea umbali mrefu kutoka kijijini hapo hadi kwenda shule iliyoko umbali wa kilometa 18.
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao wameeleza kuwa kutokana na umbali uliyokuwepo walilazimika kuwapangishia watoto wao nyumba karibu na shule maarufu kama mageto hali iliyoonekana kwamba bado ni changamoto hasa kwa usalama wa watoto wa kike kubakwa na watoto wa kiume kujiunga na makundi mabaya kwa kuwa hakukuwa na uangalizi wa wazazi.

Lusingi Sitta meneja wa CRDB kanda ya ziwa amesema umekuwa ni utaratibu wa Bank hiyo kutenga asilimia moja ya faida yao kwa mwaka kuirejesha katika kusaidia jamii katika huduma mbalimbali za kijamii kama vile afya, elimu miongoni mwa maeneo mengine.
ameongeza kuwa baada ya kupokea maombi kutoka halmashauri ya Bunda DC waliona ni vema kushiriki hivyo leo wamekabidhi meza arobaini na viti vyake ambavyo wanaamini vitakuwa msaada kwa shule hiyo.
Akipokea msaada huo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bunda George Stanley Mbilinyi ameishukuru serikali kujenga shule karibu na kupunguza adha waliyokuwa wakiipata wanafunzi kwa kutembea zaidi ya kilometa 18 hali iliyokuwa inapelekea hatari hasa kwa watoto wa kike na wengine kuacha shule.
Aidha ameishukuru Bank ya CRDB kwa msaada walioutoa ambapo amesema meza na viti walivyokabidhi leo vitasaidia kupunguza changamoto katika shule hiyo ambayo ni mpya.