Mazingira FM

Jamii yahimizwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

14 November 2025, 12:19 pm

Afisa Kilimo, Elton Dickson Mtani,akiwa studio za radio Mazingira fm ,picha na Thomas Masalu

Afisa Kilimo, Elton Dickson Mtani, jamii inapaswa kupunguza matumizi ya mbolea za viwandani, kuacha ukataji miti hovyo na kuepuka uharibifu wa vyanzo vya maji, ili kulinda mazingira.

Na Catherine Msafiri,

Jamii imetakiwa kutunza mazingira na kupunguza shughuli za kibinadamu zinazochangia uharibifu wa mazingira ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wito huo umetolewa na Afisa Kilimo, Elton Dickson Mtani, wakati akizungumza katika kipindi cha Uhifadhi kinachorushwa na Radio Mazingira FM, wakati wa utambulisho wa mradi mpya wa Land Concern for Sustainable Livelihood (LCSL).

Mtani amesema jamii inapaswa kupunguza matumizi ya mbolea za viwandani, kuacha ukataji miti hovyo na kuepuka uharibifu wa vyanzo vya maji, ili kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Sauti ya Afisa Kilimo, Elton Dickson Mtani

Kwa upande wake Johnson Kitambi, Afisa Mradi kutoka shirika lisilo la kiserikali Grain to Grow Foundation (GGF)linalosimamia utekelezaji wa mradi huo, alisema LCSL utatoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wakazi wa vijiji vilivyopo katika wilaya za Butiama na Rorya.

Johnson Kitambi, Afisa Mradi kutoka shirika lisilo la kiserikali Grain to Grow Foundation (GGF),akiwa studio za radio Mazingira FM, Picha na Thomas Masalu

Amefafanua kuwa mradi huo utahusisha shughuli mbalimbali kama upandaji miti, uanzishaji wa vikundi vya uhifadhi, na matumizi ya mbinu endelevu za kilimo rafiki kwa mazingira ili kuongeza tija bila kuharibu ardhi.

Sauti ya Johnson Kitambi, Afisa Mradi kutoka shirika Grain to Grow Foundation (GGF)

Kupitia utekelezaji wa mradi wa Land Concern for Sustainable Livelihood (LCSL), jamii katika wilaya za Butiama na Rorya inatarajiwa kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.