Mazingira FM

DC Kaminyoge: “ukimaliza kupiga kura rudi nyumbani”

27 October 2025, 8:53 pm

Wananchi baada ya kupiga kura wanarejea majumbani mwao kwa utulivu, ili kuepusha mikusanyiko isiyo ya lazima katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.

Na Thomas Masalu

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge, amewatoa hofu wananchi wa wilaya hiyo kuhusu hali ya usalama kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, akisisitiza kuwa maandalizi yote ya kiusalama yamekamilika na Wilaya ya Bunda ipo katika hali ya utulivu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mhe. Kaminyoge amesema vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu na bila vitisho vyovyote kwa wananchi watakaoshiriki katika zoezi hilo muhimu la kidemokrasia.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge,

Aidha, Mhe. Kaminyoge ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Bunda kuhakikisha kuwa baada ya kupiga kura wanarejea majumbani mwao kwa utulivu, ili kuepusha mikusanyiko isiyo ya lazima katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.

Amesema hatua hiyo itasaidia kudumisha amani na kurahisisha kazi ya wasimamizi wa uchaguzi pamoja na vyombo vya ulinzi vinavyohakikisha kila kitu kinaenda kwa utaratibu uliowekwa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge,