Mazingira FM
Mazingira FM
20 October 2025, 6:36 pm

Ujenzi huo umewezeshwa na Polish Aid na Foundation Kiabakari, na sasa kituo kina uwezo wa kuhudumia watoto 160 kwa kutoa malezi, elimu, ushauri nasaha na ulinzi wa kijamii.
Na Thedy Thomas
Katika juhudi za kulinda na kuwahudumia watoto waliokumbwa na ukatili wa kijinsia, kituo cha Hope for Girls and Women Tanzania kilichopo Kiabakari, wilayani Butiama, mkoani Mara, kimezindua makazi ya kudumu kwa watoto. Hatua hiyo imeleta matumaini mapya kwa watoto hao ambao awali walikuwa wakiishi katika nyumba za kupanga kwa muda mrefu. Ujenzi huo umewezekana kupitia ufadhili wa Polish Aid na Foundation Kiabakari, na sasa kituo kina uwezo wa kuhudumia watoto 160 kwa kutoa malezi, elimu, ushauri nasaha na ulinzi wa kijamii.

Uzinduzi wa nyumba hizo umefanywa na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Sergiusz Wolski, ambaye amepongeza juhudi za taasisi hiyo katika kuhakikisha watoto wa kike wanaishi katika mazingira salama.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Tecla Mkuchika, amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kuwalea watoto katika mazingira bora na kuzuia vitendo vya ukatili.
Kaimu Mkurugenzi wa kituo, Domina Walter Mabobe, amesema lengo la kuanzisha nyumba hiyo ni kuwasaidia watoto wanaopitia ukatili wa kijinsia. Amebainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ujenzi wa madarasa mawili, karakana mbili, jengo la utawala, bwalo la chakula lenye jiko, mabweni mawili yenye uwezo wa watoto 80 kila moja, na choo cha nje chenye matundu matano.
Hata hivyo, Mabobe ameeleza kuwa bado kuna changamoto zinazokwamisha jitihada za kukabiliana na ukatili, ikiwemo upungufu wa rasilimali na uhitaji wa msaada zaidi kutoka kwa wadau.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwel, amewashukuru viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo kwa mchango wao kufanikisha mradi huo.
kupitia risala ya watoto wanaopata malezi katika kituo hicho wamesema ujenzi wa makazi hayo mapya umeleta utulivu na usalama kwao, kwani sasa wanaishi bila hofu.
Ujenzi huo umeongeza imani ya jamii katika juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na kuwatengenezea mazingira bora kwa maisha yao ya baadaye.