Mazingira FM

TAWA yaweka mikakati kukabili wanyamapori wakali

12 October 2025, 1:48 pm

Afisa Wanyamapori kutoka TAWA, Bw. Lusato Masinde akiwa studio za radio Mazingira FM,picha na Joseph Makori

Bw. Lusato Masinde, amesema ongezeko la migongano kati ya binadamu na wanyamapori linachangiwa na upanuzi wa makazi ya binadamu, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na uharibifu wa mazingira ya asili ya wanyama hao.

Na Catherine Msafiri

Wakala wa Huduma za Wanyamapori Tanzania (TAWA) umeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wanaoathiri maisha na mali za wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi.

Akizungumza kwenye kipindi cha uhifadhi na utalii kupitia radio Mazingira FM, Afisa Wanyamapori kutoka TAWA, Bw.Lusato Masinde, amesema kuwa ongezeko la migongano kati ya binadamu na wanyamapori linachangiwa na upanuzi wa makazi ya binadamu, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na uharibifu wa mazingira ya asili ya wanyama hao.

Sauti ya Afisa Wanyamapori kutoka TAWA, Bw. Lusato Masinde

Aidha, Bw. Masinde amesema tatizo la wanyamapori wakali na waharibifu limeendelea kuathiri maeneo kadhaa nchini, hasa katika vijiji vinavyopakana na hifadhi.

Bw. Masinde ameeleza kuwa TAWA imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kudhibiti hali hiyo, ikiwemo uhamishaji wa wanyama hatarishi (translocation), utumiaji wa vizuizi vya asili na teknolojia, pamoja na elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kukabiliana na wanyamapori bila kutumia nguvu.

Sauti ya Afisa Wanyamapori kutoka TAWA, Bw. Lusato Masinde

Ametoa wito kwa wananchi kutunza mazingira na kuepuka kuingilia maeneo ya hifadhi, akisisitiza kuwa kila mtu ana jukumu la kulinda wanyamapori.