Mazingira FM
Mazingira FM
3 October 2025, 6:16 pm

Mwenyekiti wa wazungumzaji wa lugha ya kiesperanto Tanzania, Mramba Simba Nyamkinda aahidi ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 5 wanaosoma lugha hiyo watakaofanya vizuri kwenye mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka huu.
Na Catherine Msafiri
Jumla ya wanafunzi 108 wamehitimu kidato cha nne katika shule ya Sekondari Esperanto mwaka 2025. Kati ya idadi hiyo, wanafunzi wa kike ni 65 na wavulana43. Wahitimu hao ni sehemu ya wanafunzi 132 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2022.
Wakisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi katika mahafali ya 11 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2012, wanafunzi hao wamesema kuwa wanafunzi 24 hawakumaliza masomo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro na baadhi yao kuhamia shule nyingine.

Katika risala hiyo, wahitimu walitaja changamoto zinazokabili shule hiyo kuwa ni pamoja na uhaba wa viwanja vya michezo na vifaa,changamoto ya uzio, upungufu wa matundu ya vyoo na maji.
Aidha wanafunzi hao wamebainisha mafanikio waliyoyapata katika shule hiyo huku wakitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuongeza miundombinu ya madarasa, Mramba Simba aliyekuwa diwani wa kata ya Ketare kupitia shirika la Mazingira kwa ufadhili wa miradi mbalimbali na mwalimu wa lugha ya Esperanto.
Akijibu risala hiyo mgeni rasmi ambaye ni mwenyekiti wa shirika la Mazingira na mlezi wa shule ya esperanto sekondari Mramba Simba Nyamkinda ambaye pia ni mwenyekiti wa wazungumzaji wa lugha ya kiesperanto Tanzania amesema watatoa zawadi ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 5 wanaosoma lugha hiyo watakaofanya vizuri kwenye mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka huu.
Ameahidi kuelendea kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi katika shule hiyo,akibainisha kufikia mwakani watakuwa wanatumia nishati mbadala.