Mazingira FM
Mazingira FM
28 September 2025, 2:46 pm

Iwapo mgombea atakutana na vitendo vya kuombwa rushwa atoe taarifa TAKUKURU ili wachunguze na kubaini na kuchukua hatua.
Na Adelinus Banenwa
Wito umetolewa kwa wagombea wa nafasi za Urais Ubunge au Udiwani ambao wanaombwa rushwa na wapiga kura kutoa taariifa kwa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU ili sheria ichukue mkondo wake.
Hayo yamesemwa na Restuta Kessy ambaye ni mwanasheria wa TAKUKURU mkoa wa Mara wakati akizungumza kupitia kipindi cha Ufahamu wa sheria kinachorushwa na Mazingira FM ambapo amesema iwapo mgombea atakutana na vitendo vya kuombwa rushwa atoe taarifa TAKUKURU ili wachunguze na kubaini na kuchukua hatua.
Restuta amesema ni wazi kuwa katika kuchunguza lengo ni kubaini iwapo anayeomba rushwa kweli ni mpiga kura, amejiandikisha, lakini endapo muombwa rushwa hatotoa taarifa na akampatia fedha hiyo au hongo basi wote wawili watahesabika kuwa na makosa kwa mujibu wa sheria.
Aidha Bi Restuta amewaomba wananchi kuacha woga katika utoaji wa taarifa za matukio ya rushwa katika uchaguzi kwa kuwa sheria zipo za kuwalinda watoa taarifa na mashahidi na hata kama akijulikana bado TAKUKURU itatumia sheria kumlinda mtoa taarifa au shahidi kuliko kuacha vitendo vya rushwa kuendelea katiak kipindi hiki cha uchaguzi.

Kwa upande mwingine Eunice Kiwia Afisa TAKUKURU mkoa wa Mara ametoa rai kwa wananchi kupata elimu ya madhara ya rushwa na namna wanavyoweza kusaidiana na TAKUKURU kupitia program ya Takukuru rafiki ili kukomesha matukio na vitendo vya rushwa.