Mazingira FM
Mazingira FM
20 September 2025, 7:24 pm

Amesema endapo atachaguliwa kuwa diwani atahakikisha soko hilo linafanya kazi muda wote.
Na Adelinus Banenwa.
David Nyabende Thomas mgombea udiwani kata ya Nyasura kupitia chama cha Ukombozi wa Umma CHAUMA amewataka wananchi kwenda kumpigia kura katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, 29, 2025 ili aweze kuwaletea maendeleo wananchi wa kata hiyo.
David ameyasema hayo leo katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi kata ya Nyasura kwa chama cha CHAUMMA ambapo amesema pamoja na mambo mengine atahakikisha suala la miundombinu ya Barabara katika mitaa yote ya kata ya Nyasura zinapitika
Amewaomba wananchi kumuunga mkono na kumuamini ili akalete mapinduzi makubwa kuanzia halmashauri ya mji wa Bunda na kata ya Nyasura katika kuleta maendeleo kwa kuwa nia anayo, uwezo anao na Elimu anayo
.

Akigusia soko la Manjebe David amesema endapo atachaguliwa kuwa diwani atahakikisha soko hilo linafanya kazi muda wote na ikiwezekana hata bidhaa kubwa kama ndizi, mahindi, mchele na bidhaa nyingine.
Aidha amesema atasimamia sekta ya afya akigusia kusimamia sera ya afya juu ya watoto chini ya miaka mitano kupata huduma bure ambapo amesema kwa kipindi hiki ukienda hospitali unaambiwa hakuna dawa.

Ameongeza kuwa endapo akipata udiwani atahakikisha inapatikana ofisi ya kata itayojumisha ofisi za serikali ambapo itakuwepo ofisi ya mtendaji na idara zake pamoja na ukumbi wa mkutano pia itatengwa siku maalumu kwa wiki ya diwani kusikiliza changamoto za wananchi.
Awali mwenyekiti wa chama hicho kwa wilaya ya Bunda Mwira Sanjawa Mwira ambaye pia ni mgombea udiwani kata ya Bunda mjini amesema kuna kila sababu ya kuwachagua wagombea wa chama hicho kutokana na dhamira ya dhati waliyonayo ya kuwatumikia wananchi
Mwira ameongeza kuwa endapo wakienda halmashauri na wakashindwa kutekeleza waliyoahidi basi wananchi wanayo haki ya kuwahoji.