Mazingira FM
Mazingira FM
15 September 2025, 10:53 pm

Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mtambi amesisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za pamoja za uhifadhi, pamoja na kuendeleza mshikamano baina ya jamii zinazozunguka bonde hilo.
Na Catherine Msafiri,
Maadhimisho ya Mara Day yamehitimishwa leo 15 septemba 2025 katika viwanja vya Mwenge, wilayani Butiama, mkoani Mara.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi, ambaye amewaongoza wageni mbalimbali katika kuadhimisha siku hiyo .
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali pamoja na viongozi kutoka nchi jirani ya Kenya na wenyeji kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Tukio hilo limekuwa jukwaa la kuhimiza ushirikiano wa kikanda katika kulinda na kuhifadhi mazingira ya Bonde la Mara, ambalo ni rasilimali muhimu kwa mataifa yote mawili.
Katika hotuba yake, Kanali Mtambi amebainisha kuwa miti 8000 imepandwa wakati wa maadhimisho hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za pamoja za uhifadhi, pamoja na kuendeleza mshikamano baina ya jamii zinazozunguka bonde la mto Mara.
Mapema akifanya mazungumzo na redio mazingira Bi. Sawiche Wamunza kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania, ameeleza namna shirika hilo linavyoshiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira ya Bonde la Mto Mara.
Amesema kuwa kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, UNDP imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha uhifadhi endelevu wa vyanzo vya maji na rasilimali za asili zinazotegemewa na maelfu ya wananchi.
Bi. Wamunza amebainisha kuwa, kama sehemu ya maadhimisho ya Mara Day mwaka huu, UNDP kwa kushirikiana na washirika wake wamepanda miti katika maeneo mbalimbali ya Bonde la Mara ikiwa ni jitihada za kukabiliana na uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maadhimisho ya Mara day kwa mwaka huu 2025 yamebebwa na kauli mbiu isemayo “hifadhi mto Mara linda uhai”.