Mazingira FM
Mazingira FM
1 September 2025, 7:41 pm

Ameahidi huduma za afya bure kwa wananchi bila gharama zozote, ajira kwa wasomi katika sekta za elimu na uvuvi, pamoja na elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Na Adelinus Banenwa
Mgombea wa Urais kupitia Chama cha Wananchi CUF, Gombo Samandito Gombo, pamoja na mgombea mwenza wake Husna Abdullah, wamefanya mkutano wa kampeni katika mji wa Bunda mkoani Mara.
Akihutubia wananchi, Gombo amesema licha ya taifa kuwa na rasilimali nyingi, bado wananchi wanaendelea kuishi katika hali ya umasikini, hali ambayo amesema imesababishwa na chama cha mapinduzi kilichopo madarakani. Amesema matatizo makuu ya Bunda bado ni yale yaliyowahi kuelezwa na Mwalimu Julius Nyerere ambayo ni ujinga, maradhi na umasikini.

Mgombea huyo ameahidi huduma za afya bure kwa wananchi bila gharama zozote, ajira kwa wasomi katika sekta za elimu na uvuvi, pamoja na elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Aidha, amesisitiza kuwa serikali ya CUF itakomesha rushwa na ufisadi kwa kuwawajibisha wale wote watakaokutwa wakihujumu mali za umma.
Katika sera zake, Gombo amesema kila mtumishi wa umma ataajiriwa akiwa na hati ya kiwanja na nyumba ya kuishi, huku huduma za serikali zikiletwa karibu kupitia afisa mtendaji wa kata. Pia ameahidi wananchi kuunganishiwa umeme na maji bila kulipia gharama za awali, na kuanzisha mchakato wa katiba mpya ndani ya siku mia moja za kwanza za uongozi wake.
Akihitimisha hotuba yake, Gombo amesema rasilimali na fedha za kuwaletea wananchi maendeleo zipo, akiahidi usawa wa umiliki wa ardhi kati ya wanawake na wanaume, na kuondoa utitiri wa kodi kwa kuweka kodi moja tu inayolipwa mara moja kwa mwaka.