Mazingira FM
Mazingira FM
31 August 2025, 7:26 am

Amenusurika kuliwa na mamba wakati akiwa katika shughuli za uvuvi wa samaki.
Na Edward Lucas.
Aloyce Komanya (32), mkazi wa mtaa wa Bushigwamala, kata ya Guta katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, mkoani Mara, amenusurika kuliwa na mamba wakati akiwa katika shughuli za uvuvi wa samaki katika eneo la Tairo, kata ya Guta.
Akisimulia tukio hilo, Aloyce ambaye pia ni mhudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) katika mtaa wa Bushigwamala, alisema kuwa tukio hilo lilitokea asubuhi ya tarehe 29 Agosti 2025, alipokuwa akivua samaki pamoja na baba yake mzazi.
Komanya Kinasa, ambaye ni baba mzazi wa Aloyce, alisema kuwa alisikia kilio cha mwanae na alipogeuka alimkuta akiwa ameshikwa na mamba.

Awali Mazingira FM ilifuatilia tukio hili na kufika katika Hospitali ya Bunda (Bunda DDH), ambapo ilibainika kuwa mgonjwa alikuwa tayari ameondoka.
Uongozi wa hospitali ulithibitisha kuwa walimpokea Aloyce Komanya, wakampatia huduma ya awali, na baadaye familia yake iliomba kuondoka ili kuendelea na matibabu nyumbani. Hospitali iliridhia kutokana na hali ya mgonjwa kuwa imetulia.
Baadhi ya mashuhuda waliokuwa karibu na eneo la tukio waliiambia Mazingira FM kuwa walikuwa wamesikia kelele kutoka eneo la ziwani lakini hawakuzitilia maanani, wakidhani ni kelele za kawaida kutoka kwa wavuvi.
Wakazi wa eneo hilo wametoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuzuia matukio kama hayo, ikiwemo kutoa elimu ya usalama na kuweka tahadhari kwenye maeneo hatarishi ya ziwa.