Mazingira FM
Mazingira FM
20 August 2025, 10:31 pm

Tukio hilo lilitokea jana tarehe 19 Augost 2025, majira ya saa 12:00 jioni, wakati Lutamula na wenzake walipokuwa katika shughuli ya ukarabati wa duara
Na Edward Lucas.
Mchimbaji Afukiwa na Kifusi Katika Mgodi wa Dhahabu Juma Lutamula (33), mkazi wa Katolo mkoani Geita, amefukiwa na kifusi akiwa katika shughuli za ujenzi wa duara la uchimbaji katika mgodi wa Walwa, eneo la Kinyambwiga, Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara.
Tukio hilo lilitokea jana tarehe 19 Augost 2025, majira ya saa 12:00 jioni, wakati Lutamula na wenzake walipokuwa katika shughuli ya ukarabati wa duara lenye urefu wa takribani futi 70, ambapo hadi wakati wa ajali walikuwa wamefikia futi 30 kwa mujibu wa manusura wa tukio hilo, Sayi Kiloshimba.

Operesheni ya uokoaji inaendelea kwa ushirikiano wa wachimbaji wenzake pamoja na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara. Hadi kufikia saa 9 usiku wa jana, baadhi ya vijana wa kikosi hicho walieleza kuwa walikuwa bado wanaweza kuwasiliana na Juma akiwa hai, lakini kazi ya uokoaji ililazimika kusitishwa kwa muda kutokana na hatari ya kuporomoka kwa maduara mengine.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi Augustine Magere, amewataka wananchi kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano wakati juhudi za kumuokoa Lutamula zikiendelea.