Mazingira FM
Mazingira FM
13 August 2025, 7:12 pm

Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za Mkendo, Shaabani na Musoma–Saanane, Ujenzi wa Soko Kuu la Nyasho na Kituo cha Mabasi cha Bweri.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa wilaya ya Musoma Mhe Juma Chikoka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia Musoma miradi muhimu itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 19.975 (bila VAT) na ambayo inalenga kuboresha miundombinu ya barabara, soko na kituo cha mabasi.
Akizungumza na wakazi wa musoma kupitia radio mazingira fm kwenye kipindi cha asubuhi leo Mhe Chikoka amesema miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za Mkendo, Shaabani na Musoma–Saanane, Ujenzi wa Soko Kuu la Nyasho na Kituo cha Mabasi cha Bweri.

Mhe Chikoka amesema miradi hiyo ikikamilika itabadilisha mandhari ya mji wa Musoma, kuwa kivutio kipya na kuchochea uchumi wa eneo hilo, sambamba na kutoa ajira kwa wananchi na kuongeza fursa za kiuchumi kutokana na kuwa mji wa Musoma ni mji wa kibiashara.
Mhe Chikoka amesema miradi hii imezingatia maeneo ambayo serikali imewekeza fedha nyingi na ni maeneo ambayo yanatoa huduma kwa wananchi ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma ambapo amehaidi kuwa kufikia mwezi November wakazi wa musoma na mkoa wa mara kwa ujumla hawatakuwa na sababu ya kwenda mwanza kupanda usafiri wa ndege badala yake huduma hiyo itakuwa ikipatikana Musoma.