Mazingira FM

Mwingine ajeruhi kisha kujinyonga Bunda

25 July 2025, 7:36 am

Siku moja baada ya Mazingira FM kuripoti tukio la mama kujinyonga Bunda katika mtaa wa Migungani kata ya Bunda Stoo mwingine tena kujeruhi kisha kujinyonga.

Na Adelinus Banenwa

Mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Spareas Magaso (61), mkazi wa mtaa wa Idara ya Maji, kata ya Bunda Stoo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, amefariki dunia kwa kujinyonga baada ya kumshambulia kwa mapanga mwanamke anayedaiwa kuwa mpenzi wake, Rehema Makongoro (47), mkazi wa mtaa wa Kabusure, kata ya Nyamakokoto, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Tukio hilo limetokea alfajiri ya saa 11, Julai 24, 2025, nyumbani kwa Rehema.

Kwa mujibu wa Rechel Charles, mpangaji katika nyumba hiyo, alisikia kelele za Rehema akiomba msaada.

Alipochungulia dirishani, alimuona Spareas akimshambulia Rehema kwa mapanga.

Kutokana na hofu ya kudhuriwa, Rechel hakuthubutu kutoka nje, bali alianza kupiga kelele ili kuwaamsha majirani.

Sauti ya Rechel Charles

Mke wa marehemu, Bi. Prisca Spareas, ameiambia redio Mazingira FM kuwa alipokea taarifa hizo kwa mshtuko mkubwa.

Asubuhi hiyo alipokea simu kutoka kwa namba ya mume wake, lakini aliyekuwa akizungumza ni mwanamke aliyetoa taarifa za Magaso kumjeruhi mtu na kisha kujinyonga.

Awali hakuliamini jambo hilo, hadi pale jirani yake alipothibitisha kuwa ni kweli mumewe ametekeleza tukio hilo la kusikitisha.

Sauti ya Mke wa marehemu, Bi. Prisca Spareas

Mwenyekiti wa mtaa wa Kabusure, Bw. Lucas Yona Masunga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika mtaa wake.

Amesema kuwa alifahamishwa na mjumbe wa serikali ya mtaa anayeishi jirani na eneo la tukio, na alipoenda kufika mwenyewe na kushuhudia hali hiyo, aliwajulisha askari wa Jeshi la Polisi ambao walifika haraka eneo la tukio.

Kwa mujibu wa Masunga, majeruhi Rehema alikimbizwa katika Hospitali ya Bunda (Bunda DDH) kwa ajili ya matibabu, huku mwili wa marehemu Magaso ukihamishiwa katika mochwari ya Kituo cha Afya Bunda.

Mwili huo tayari umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Sauti ya Mwenyekiti wa mtaa wa Kabusure, Bw. Lucas Yona Masunga