Mazingira FM
Mazingira FM
30 June 2025, 12:25 pm

Bulaya amesema ameamua kurejea nyumbani baada ya kutafakari kwa kina, akieleza kuwa alihamia CHADEMA kwa kile alichokiita “mkopo wa kisiasa.”
Na Adelinus Banenwa
Aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunda Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Esther Bulaya, amerejea rasmi Chama Cha Mapinduzi, CCM, na kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge wa jimbo hilo kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo katika ofisi za CCM Wilaya ya Bunda, Bulaya amesema ameamua kurejea nyumbani baada ya kutafakari kwa kina, akieleza kuwa alihamia CHADEMA kwa kile alichokiita “mkopo wa kisiasa.”
Amesema dhamira yake sasa ni kushirikiana na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Bunda, akiongeza kuwa anaamini bado ana mchango mkubwa wa kuutoa kwa taifa kupitia CCM.

Katika hatua hiyo, ushindani wa kinyang’anyiro cha ubunge wa Bunda Mjini ndani ya CCM umeongezeka, baada ya mtoto wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Kambarage wa Wasira, naye kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Aidha, aliyekuwa mbunge wa sasa, Robert Maboto, amejitosa tena kutetea nafasi hiyo na tayari amekamilisha taratibu za awali za uchukuaji na ulejeshaji fomu.
Hali hiyo imeweka wazi kuwa kura za maoni ndani ya CCM Bunda Mjini zitakuwa na mvutano mkali, huku kila mgombea akijinasibu kuwa na uwezo wa kuliletea jimbo hilo maendeleo endelevu