Mazingira FM
Mazingira FM
20 June 2025, 6:58 am

Mradi huo una urefu wa kilometa 33 kuanzia kwenye tenki mpaka Nyamuswa ambapo wananchi wote wanaopitiwa na mradi huo watanufaika.
Na Adelinus Banenwa
Wananchi wapatao elfu 51 wanatarajiwa kunufaika na upanuzi wa mradi wa Butiama Nyamuswa ambao unatokea katika mradi mama wa Mugango Kiabakari hadi Butiama.
Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo Mwenyekiti wa bodi ya BUWSSA ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Joshua Mirumbe amesema kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 15 ya utekelezaji.
Mirumbe amesema wanaishukuru serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha fedha shilingi bilion 8.3 kutekeleza mradi huo.

Mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda BUWSSA ambapo una urefu wa kilometa 33 kuanzia kwenye tenki mpaka Nyamuswa ambapo wananchi wote wanaopitiwa na mradi huo watanufaika na huduma ya maji hayo.
Michael Shayo Mhandisi kutoka BUWSSA amesema hadi sasa umechimbwa mtaro karibu kilometa 8 na utekelezaji wa mradi huo utakuwa na hatua mbalimbali ikiwemo junzi wa matenki ya kupokea maji kutoka kwenye chanzo kikuu na usambazaji wa mtandao wa mabomba kilometa hizo 33.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa BUWSSA Denis Ashrafu amesema BUWSSA wameanza utekelezaji wa miradi huo tangu mwezi wa pili mwaka huu waliposaini mkataba na unatarajiwa kukamilika mwakani mwezi Januari huku akiwahakikishia wananchi wa kata ya Nyamuswa na viunga vyake vyote kuwa wanakwenda kunufaika kwa kupata maji safi na salama baada ya mradi huo kukamilika.
Kwa upande wao wananchi wa kata ya Nyamuswa wameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo wa maji huku wakiomba mradi huo kutekelezwa kwa haraka ili kupunguza changamoto za maji wanazozipata hasa kipindi cha kiangazi.