Mazingira FM

Wananchi Bunda wazungumzia umuhimu wa kuchangia damu

14 June 2025, 10:15 am

Pakti za damu Picha kutokea mtandaoni

Mara nyingine wagonjwa wanaohitaji damu hukosa huduma hiyo kwa wakati kutokana na ucheleweshaji, au mfumo usio wa wazi katika benki ya damu.

Na Fabian Ndomi

Baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, hasa kutoka kata za Nyamakokoto na Kabarimu, wameeleza kuwa ni muhimu kwa kila mtu kujitoa kuchangia damu, ili kuokoa maisha ya wengine.

Wakazi hao wamesema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na wizara ya afya kupitia mpango wa Damu Salama, bado kuna changamoto katika mfumo wa utoaji damu kwa wahitaji.

Wananchi hao wameeleza kuwa mara nyingine wagonjwa wanaohitaji damu hukosa huduma hiyo kwa wakati kutokana na ucheleweshaji, au mfumo usio wa wazi katika benki ya damu.

Pia, wamesisitiza kuwa wachangiaji wanahitaji motisha, kama vile elimu ya afya na lishe bora baada ya kuchangia damu, ili waweze kuona thamani ya kile wanachokifanya na kuendelea kuwa sehemu ya mfumo wa damu salama.

Licha ya kuwa mwamko umeongezeka kwa baadhi ya watu kujitokeza kuchangia, bado wengine wana wasiwasi na hofu kwa sababu elimu ya kutosha kuhusu uchangiaji damu salama haijawafikia watu wote.

Baadhi wamelalamika kuwa hata wanapojitokeza kuchangia mara kwa mara, bado kuna ugumu mkubwa wanapohitaji damu wao au ndugu zao.

Wengine wameeleza kuwa kuna matukio ya watu kuombwa hongo ili kupata damu hospitalini, hali ambayo imezua masikitiko.

Sauti ya baadhi ya wanawake Bunda wakieleza maoni yao kuhusu siku ya mchangia damu

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Changia Damu, Leta Matumaini Pamoja Tunaokoa Maisha.”
Huduma za kuchangia damu zinapatikana katika vituo vya Damu Salama vya kanda, hospitali za rufaa, hospitali za mikoa na wilaya, kambi za jeshi pamoja na maeneo ya wazi yanayoruhusiwa.