Mazingira FM

Bunda: Aliwa na mamba akiwa kwenye uvuvi Ziwa Victoria

25 March 2025, 10:35 pm

Afariki dunia kwa kuliwa na mamba baada ya kumkamata akiwa anaendelea na uvuvi wa samaki kando ya ziwa Victoria.. sehemu ndogo tu ya mwili imepatikana familia wazika

Na Thomas Masalu

Mashiku Mihayo (49) mkazi wa mtaa wa Guta Mjini amefariki dunia kwa kuliwa na mamba wakati akiwa katika shughuli za uvuvi wa samaki kando ya ziwa Victoria eneo la Guta wilaya ya Bunda mkoa wa Mara ambapo tukio hilo limetokea 23 March 2025 siku ya jumapili.

Akizungumzia tukio hilo, Janes Mihayo, mdogo wa marehemu, amesema kuwa ndugu yao aliondoka nyumbani siku ya Jumapili, majira ya saa 3:00 asubuhi akielekea katika shughuli za uvuvi wa samaki ambapo hadi kufikia usiku saa 2:00 hakuonekana nyumbani ndipo juhudi za kumtafuta zilianza

Amesema baada ya kufika eneo alilokuwa akifanyia shughuli za uvuvi walikuta nguo, simu, na vifaa vyake vya uvuvi na hivyo kuanza zoezi la kumtafuta kwa siku hiyo bila mafanikio hadi leo majira ya saa 3:00 asubuhi walipofanikiwa kupata sehemu ya mwili ambao ni mguu wa kushoto wa marehemu.

Sauti ya Janes Mihayo

Kennedy Mihayo, ambaye pia ni mdogo wa marehemu, amesema zoezi la utafutaji halijaishia hapo, na kwamba familia wataendelea na juhudi za kutafuta masalia mengine, hata hivyo sehemu ya mwili waliyoipata wameamua kuizika.

Kennedy Mihayo, mdogo wa marehemu akizungumza na radio Mazingira Fm. Picha na Edward Lucas
Kennedy Mihayo akisimulia tukio

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Guta Mjini, ndugu Stephen Malweta amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwasisitiza wananchi hususani wavuvi kuchukua tahadhari kwa kufanya uvuvi salama na kuepuka uvuvi hatarishi wa kutumia ‘mbigo’ kwani kumekuwa na matukio ya kujirudia rudia na kwamba kwa upande wao wataendelea kuchukua hatua

Steven Malweta, mwenyekiti mtaa wa Guta Mjini