

23 March 2025, 12:24 pm
Mwanamke aliyedaiwa kumchoma mwanae kiganja cha mkono kwenye jiko la mkaa atiwa mbaroni wananchi wataka kumshushia kipigo.
Na Adelinus Banenwa
Ni Neema Musimu John mkazi wa mtaa wa Mapinduzi kata ya Bunda mjini mkoani Mara ambaye inadaiwa kumchoma moto kwenye kiganja cha mkono mtoto wake wa kumzaa kwa sababu ya kujisaidia kwenye nguo amenusurika kipigo baada ya kutiwa mbaroni na wananchi.
Wananchi hao wakiwa wanaonekana kuwa na hasira kutokana na kitendo alichokifanya mwanamke huyo walikusanyika katika ofisi ya serikali ya mtaa wakimtaka mwenyekiti awakabidhi mwanamke huyo na wao wamchome mikono kama yeye alivyomfanya mtoto wake.
Baadhi ya mashuhua wameiambia Mazingira Fm kuwa jirani yao huyo alimchoma mtoto wake huyo siku ya tarehe 18 March 2025 kwa kosa la kujisaidia kwenye nguo na imekuwa ni kawaida yake kutoa adhabu za kupindukia kwa mtoto huyo huku akiwatishia majirani hao kutoa taarifa
Mwenyekiti wa mtaa mapinduzi kata ya Bunda mjini Daniel Yapanda amesema mwanamke huyo wamemkamata majira ya jioni baada ya kufika nyumbani kwake akitokea jijini Mwanza anakodai alienda kufuata biashara, kisha kumfikisha ofisi za serikali za mitaa ambapo utaratibu ni kumpeleka kituo cha polisi.
Mwenyekiti Yapanda ametoa rai kwa wananchi kujenga tabia ya kutoa taarifa za matukio ya kikatili yanayofanyika katika familia ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa wahanga wa ukatili huo
Naye Lucia John Tabuse katibu wa jumuiya ya wazazi chama cha mapinduzi wilaya ya Bunda ambaye alimsaidia mtoto huyo kupata matibabu kwa kushirikiana na viongozi wengine wa mtaa na kata, amewataka wazazi hasa wanawake kuwa karibu na watoto wao ili kutambua changamoto walizonazo badala ya kutoa adhabu za kikatili kwa matatizo yanayoweza kushughulikiwa kiafya.
Ikumbukwe tukio la mtoto wa umri wa miaka 5 kubainika ameunguzwa kiganja cha mkono liliibuliwa na wasamalia wema March 21, 2025 mtaa wa Mapinduzi kisha kutoa taarifa kwa viongozi ambao walichukua hatua za kumfikisha hospitali ili kupata huduma za matibabu.