

22 March 2025, 9:03 pm
Licha ya sensa ya watu na makazi ya 2022 kuonesha idadi ya wanawake ni wengi kuliko wanaume, katika nafasi za uongozi kwa ngazi za udiwani na ubunge bado kuna idadi ndogo zaidi ya uwakilishi.
By Edward Lucas
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania TAMWA kwa kushirikiana na TADIO wameendesha mafunzo kwa radio za kijamii Tanzania Bara kuandaa habari na vipindi vitakavyowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu hasa kwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa 2025.
Akizungumzia mafunzo hayo, Meneja Mipango na Mikakati TAMWA, Sylivia Daulinge amesema mafunzo hayo yanayodhaminiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Vyombo vya Habari Finland VIKES yamelenga elimu ya namna bora ya kuandaa vipindi vya usawa na ujumuishi wa masuala ya kijinsia kwa kuhakikisha wanawake hasa vijana na makundi maalumu yanapewa kipaumbele kuelekea uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Radio Tadio, Hilali Alexander Ruhundwa amesema kwa kushirikiana na TAMWA wameona wanajukumu la kufanya katika jamii kwa kuwashirikisha waandishi wa habari ili kufikisha elimu kwa jamii kuwafanya wanawake washiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao
Kwa takwimu za uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020, madiwani wanawake waliochaguliwa kwenye kata ni 260 kati ya 3,953 ambao ni sawa na asilimia 6.58 na kwa upande wa ubunge kati ya majimbo 264 wabunge wanawake waliochaguliwa kwenye majimbo ni 26 tu sawa na asilimia 9.85