

25 February 2025, 9:00 am
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini Mhe. Robert Chacha Maboto amewataka wazazi kujitolea katika kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni ili kuongeza hali ya taaluma.
Na Adelinus Banenwa
Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto amewataka wazazi kujitoa katika kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni ili kuongeza hali ya taaluma kwa shule za halmashauri ya mji wa Bunda.
Mhe Maboto amesema hayo tarehe 24 Feb 2025 katika ziara yake alipozitembelea jumla ya shule saba za sekondari za halmashauri ya mji wa Bunda kuhamasisha zoezi la uchangiaji wa chakula mashuleni.
Mhe mbunge amesema maisha ya wakati huu ni tofauti na maisha ya zamani kutokana na mabadiliko mbalimbali ambapo zamani wazazi walitegemea mifugo na mashamba lakini kwa sasa kitu pekee ambacho mzazi anaweza kumrithisha mtoto wake kikamsaidia ni elimu tu.
Mhe Mbunge ametembelea shule za sekondari za Dkt Nchimbi, Manyamanyama, Kabasa, Wariku, Guta, Nyamakokoto na shule ya Sekondari ya Bunda mjini ambapo kila shule ametoa gunia 4 za mahindi, maharage pamoja na sukari kilo 25.
Kwa upande wao wanafunzi wameshukuru jitihada za Mhe mbunge kuwakumbuka kuwaletea chakula huku wakiahidi kusoma kwa bidii na kuwa chachu ya kuwahamasisha wazazi wao kupeleka chakula mashuleni.
Baadhi ya viongozi wa maeneo husika wakizungumza katika ziara hiyo wameainisha juhudi wanazozifanya kuhakikisha wazazi wanaleta chakula shuleni ambapo hamasa hizo inaelezwa zinafanyika kupitia kwa viongozi wa kata pamoja na kamati za shule.
Afisa lishe halmashauri ya mji wa Bunda Lucy Mwalwayo amesema kushindwa kupata chakula kwa mwanafunzi kutwa nzima kuna madhara makubwa ikiwemo changamoto wa uelewa darasani, vidonda vya tumbo pamoja na upungufu wa lishe bora.