

16 February 2025, 6:37 pm
Zaidi ya Wagonjwa 1,520 Wahudumiwa Bure Katika Kambi ya Matibabu ya Macho Bunda Manyamanyama.
Na Adelinus Banenwa
Zaidi ya wagonjwa 1,520 wa macho wamehudumiwa ndani ya siku mbili kati ya tatu katika kambi maalumu ya matibabu ya macho iliyofanyika katika Hospitali ya Bunda Manyamanyama.
Akizungumza katika kambi hiyo, rais wa Chama cha Lions Clubs International, Mahamoud Rajuan, amesema kati ya wagonjwa hao, 150 wamefanyiwa upasuaji wa macho kutokana na changamoto mbalimbali walizokuwa nazo, ikiwa ni pamoja na mtoto wa jicho.
Mahamoud amewashukuru wananchi kwa kujitokeza na pia kuwashukuru wafadhili waliowezesha kufanyika kwa kambi hiyo, ambapo huduma zilikuwa bure.
Naye, Dr. Majey Majey, mganga anayehusika na huduma za matibabu ya macho na vipimo, amesema kwa siku hizo mbili wamewahudumia wagonjwa 1,520 na wanashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kupata matibabu.
Dr. Majey ameeleza kuwa matatizo ya macho yanaweza kusababishwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo aleji, mtoto wa jicho, presha ya macho, vumbi, moshi, na mengine, na hivyo wanatoa ushauri kulingana na chanzo cha ugonjwa wa kila mgonjwa.
Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa waliopata huduma katika kambi ya siku tatu wamewashukuru kwa huduma walizopata, kwani hawakudaiwa fedha yoyote kuanzia kwenye vipimo hadi upasuaji.
Kambi hiyo ya matibabu ya macho katika Hospitali ya Bunda Manyamanyama ilianza tarehe 14 Februari na kumalizika leo, tarehe 16 Februari 2025, huku matibabu yaliyotolewa ikiwa ni pamoja na huduma za vipimo, ugawaji wa miwani ya jua na kusomea, pamoja na upasuaji, yote hayo yakitolewa bure.