

15 February 2025, 7:45 pm
Serikali ya mtaa inachukua hatua muhimu katika kusimamia usalama na ustawi wa jamii katika kipindi hiki cha shughuli za uchimbaji.
Na Adelinus Banenwa
Makumi kwa mamia ya vijana kutoka maeneo mbalimbali wameshukudiwa katika viunga vya mtaa wa Zanzibar , kata ya Nyasura, halmashauri ya mji wa Bunda, kutokana na kuibuka kwa rashi ya madini ya dhahabu katika eneo hilo kwa lengo la kuanza shughuli za uchimbaji.
Mwenyekiti wa mtaa wa Zanzibar, Nyabatuli Ndege, amesema kuwa serikali ya mtaa inachukua hatua muhimu katika kusimamia usalama na ustawi wa jamii katika kipindi hiki cha shughuli za uchimbaji.
Nyabatuli amesema kuwa wanahakikisha kuwa kuna usafi, maeneo ya chakula yamewekwa mbali na maeneo ya uchimbaji, na uchimbaji wa vyoo umeanzishwa ili kudumisha afya na usalama kutokana na wingi wa watu wanaokusanyika.
Naye mtendaji wa mtaa wa Zanzibar, Bi. Grece Mwita, ameeleza kuwa halmashauri tayari imeanza kukusanya mapato kutoka kwa wachimbaji, ambapo kila kiroba cha mchanga kinachopakiwa kinatozwa shilingi 1000.
Grece amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wachimbaji kufuata utaratibu wa kisheria na kulipa mapato kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Maiga James Majanjala, mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini wi, ametoa wito kwa vijana wote kuwa watulivu na kuzingatia sheria za uchimbaji. Huku akiwahakikishia kuwa viongozi wa wachimbaji wako mstari wa mbele kuhakikisha utaratibu unafuatwa ili kuepuka migogoro na madhara yoyote.
Awali akizungumza na Mazingira fm moja ya vijana wa mwanzo kugundua uwepo wa dhahabu katika eneo hilo la Zanzibar amesema eneo hilo kwa kawaida walikuwa wanalitumia kuchimba kokoto na molamu lakini siku ya ijumaa jioni ndipo walipoona mawe yenye chembechembe za madini ya dhahabu na walipokwenda kuyasaga alipata gram 3.5 ndipo alianza kuwapa taarifa wengine