Mazingira FM

Waandishi redio jamii Kanda ya Ziwa wajengewa uwezo kuhusu marburg

11 February 2025, 7:09 am

Dr. Chikondi Khangamwa mtaalam wa jamii na tabia kutoka UNICEF

Dalili za awali za ugonjwa huu hazitofautiani sana na ugonjwa wa maralia kama vile homa kali, maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo, maumivu ya misuli, na kutapika na saa nyingine ngonjwa anaweza kutapika damu.

Na Adelinus Banenwa

Mtandaoni wa Redio za Kijamii Tanzania TADIO kwa kushirikiana na serikali pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto UNICEF wamefungua mafunzo kwa waandishi wa habari wa redio jamii Kanda ya Ziwa yenye lengo la kuwajengea uelewa waandishi hao kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa marburg.

Kaimu afisa afya mkoa wa kagera ndugu Salumu Kimbau

Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yanafanyika mjini Bukoba mkoani Kagera ambapo mlipuko wa ugonjwa huo kwa mara mbili umezuka katika wilaya ya Biharamulo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Kaimu Afisa Afya Mkoa wa Kagera Bw. Salumu Kimbau amesema serikali inatambua sana mchango wa vyombo vya habari na wanahabari katika kupeleka taarifa sahihi kwa jamii kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya zinapojitokeza kama vile magonjwa ya milipuko kama ulivyo ugonjwa wa marburg lengo ni kuondoa taharuki kwenye jamii.

Baadhi ya waandishi wa habari wa redio jamii Kanda ya Ziwa katika mafunzo mkoani Kagera

Akizungumzia ugonjwa wa marburg ndugu Kimbau amesema dalili za awali za ugonjwa huu hazitofautiani sana na ugonjwa wa maralia kama vile homa kali, maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo, maumivu ya misuli, na kutapika na saa nyingine ngonjwa anaweza kutapika damu huku hatua mbaya zaidi katika ugonjwa huu ni pale ugonjwa anapoanza kutokwa na damu sehemu za wazi za mwili wake.

Kimbau ameongeza kuwa hadi sasa ugonjwa wa Marburg hauna chanjo wala tiba isipokuwa ngonjwa anatibiwa tu dalili zinazokuwa zinajitokeza kama vile homa, maumivu ya kichwa n.k huku akisisitiza kuwa dalili za ugonjwa huu kujitokeza kati ya siku moja hadi siku 21 ambapo wahisiwa wote huwekwa karantini kwa lengo la kufuatiliwa ikiwa wameathirika na ugonjwa huo la.

Katika hatua nyingine Kimbau amesema ugonjwa huo huenezwa kwa kugusana na muathirika wa ugonjwa huo kupitia majimaji inaweza kuwa ni jssho, mate, kujamiiana, kugusa vyombo au matandiko ya mgonjwa lakini hadi sasa hakuna utafiti unaoonesha kuwa ugonjwa huo unaenezwa kwa njia ya hewa.

Naye Dr. Chikondi Khangamwa Mtaalamu wa jamii na tabia kutoka UNICEF amesema shirika hilo la umoja wa mataifa limeamua kushirikiana na serikali pamoja na TADIO kutokana na sera zao ambapo wanaamini mara nyingi kwenye majanga kama vile magonjwa ya milipuko, vita na majanga ya asili waathirika wakubwa ni watoto hivyo hata katika mlipuko huu wa ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera wamelazimika kushiriki kwa kuwa mtoto alipo basi UNICEF wapo.