

8 February 2025, 10:18 pm
Waziri Gwajima ameiagiza mikoa yote inayoongoza kwa ukeketaji nchini kutenga bajeti za kutekeleza afua za kupinga ukeketaji ikiwa ni pamoja na kuwahudumia manusura wa ukatili wa ukeketaji na ukatili mwingine.
Na Adelinus Banenwa
Waziri wa Maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalumu Dr. Doroth Gwajima ameiagiza mikoa yote inayoongoza kwa ukeketaji nchini kutenga bajeti za kutekeleza afua za kupinga ukeketaji ikiwa ni pamoja na kuwahudumia manusura wa ukatili wa ukeketaji na ukatili mwingine ikiwemo kuwawezesha watoa huduma kuwafikia wahanga kwa urahisi.
Dr Gwajima ameyasema hayo leo Feb 8, 2025 wilayani tarime kwenye maadhimisho ya siku ya kupinga ukeketaji Duniani
Maadhimisho hayo ameambatana na uzinduzi wa kituo jumuishi cha huduma kwa wahanga wa matukio ya ukatili eneo la Nyamwaga Tarime kilichogharimu shilingi milioni 186 kwa ufadhili wa shirika la umoja wa mataifa linalojihusisha na idadi ya watu duniani UNFPA ambapo lengo kuu la kituo hicho ni kutoa huduma za pamoja kwa wahanga na manusura wa ukatili ndani ya jengo moja.
Kutuo hicho tangu kilipoanza kufanya kazi mwezi July 2024 hadi sasa manusura wapatao 325 wakiwemo watoto 204 wamehudumiwa ambapo kwa mujibu wa takwimu hizo watoto ndiyo wanaofika kituoni hapo kwa wingi kupata huduma.
Kituo hicho kinatoa huduma za afya, msaada wa kisheria pamoja na ustawi wa jamii lengo likiwa ni kutoa huduma za pamoja kwa manusura wa ukatili ambapo UNFPA kadhalika wamejenga jengo kama hilo katika mkoa wa Shinyanga.
Pia Mhe Gwajima amesema mbinu mpya ya Ukeketaji imeibuka hasa maeneo ya mipakani ambapo makundi ya vijana wa kike huvushwa mipakani na kupelekwa nchi jirani kwa ajiri ya kufanyiwa ukeketaji na kisha kurudishwa nchini bila kubainika pia mangariba vivyo hivyo.
Katika kukabiliana na mbinu hizo mhe Waziri Gwajima ameelekeza vituo vyote jumuishi vikae na kuandaa taarifa yao ya pamoja itayohusisha wataalamu wa afya. Jeshi la polisi na ustawi wa jamii ili muhutasari wao uambatanishwe na MTAKUWA kisha upelekwe ofisi za wilaya kisha mkoani kisha upande kwenda wizarani na wizara zitakaa na kushauri wanasheria kufanya marekebisho ya sheria ya ukeketaji na masuala mengine kama yatakavyokuwa yamependekezwa kutoka kwenye vituo hivyo.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mara Kanal Evance Mtambi ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Tarime kupitia mapato ya ndani kujenga nyumba salama kwa ajili ya watoto wanaofanyiwa ukatili.
Pia Dr Naano kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mara ameagiza kutolewa kwa elimu Maafisa wa jeshi la polisi wanaohusika na kuhudumia wahanga wa ukatili ili wawe na mtazamo mmoja katika kushughulikia kesi hizo za ukatili.
Mark Bryan Schreiner mwakilishi mkazi wa UNFPA nchini Tanzanian amesema tatika kupambana na ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni kunahitajika juhudi za pamoja kati ya wanawake wanaume watoto vijana pamoja na serikali
Mark amesema kupitia program ya chaguo langu haki yangu imeonesha mshikamano na utayari wa serikali katika kutokomeza ukatili huo kwenye jamii.
Michael Marwa kutoka C-SEMA na Valerian Mgani kutoka ATFGM MASANGA taasisi ambazo zimejikita katika kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa akinamama na watoto hasa wenye ulemavu GBV wamesema hotuba ya Mhe Waziri wameipokea kwa mikono miwili kutokana kwa kuwa inaonesha namna serikali kwa kushirikiana na wadau wameweza kupunguza kiwango cha ukeketaji nchini na mipango itakayowezesha kuendelea kusaidia kushusha kiwango cha ukeketaji na hata kubaki asilimia 0