Mwanamke auawa na watu wasiyojulikana Bunda
20 January 2025, 8:59 am
Mwenyekiti Hamis Said Madoro “Amekutwa na majeraha katika maeneo mbalimbali mwilini mwake na amefariki wakati anapelekwa kwenye huduma za matibabu”
Na Adelinus Banenwa
Mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Akinyo Kumu (39) mkazi wa kijiji cha Nyaburundu kata Ketare halmashauri ya wilaya ya Bunda anatajwa kupigwa na watu wasiyojulikana hali iliyopelekea kifo chake.
Hamis Said Madoro mwenyekiti wa kijiji cha Nyaburundu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema tukio hilo limetokea Jan 18, 2025 majira ya saa mbili asubuhi ambapo walimkuta Akinyo akiwa chini maeneo karibu na nyumbani kwako huku akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Madoro ameongeza kuwa baada kumtambua mama huyo alitoa taarifa jeshi la polisi pia alifanya jitihada za kumfikisha zahanati iliyopo kijijini hapo ambapo jitihada hizo hazikuzaa matunda.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa wauguzi katika zahanati ya Nyaburundu walimpatia rufaa ya kwenda kituo cha afya Ikizu Nyamuswa ambapo baadaye alipokea taarifa za mama huyo kupoteza maisha.
Aidha mwenyekiti Madoro ametoa rai kwa wananchi kutojichukulia sheria mikononi huku akilaani kitendo hicho na kuliomba jeshi la polisi kuwasaka wahusika wa tukio hilo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Jitihada za kulitafuta jeshi la polisi mkoa wa Mara zinaendelea kujua chanzo cha tukio hilo Endelea kufuatilia vipindi vyetu.