Mazingira FM

Mhe Maboto atoa tabasamu kwa wanafunzi zaidi ya 500 kwa kuwanunulia vifaa vya shule

11 January 2025, 7:36 am

Zaidi ya shilingi milioni 38 zatumiwa na mbunge wa Bunda mjini Mhe Robert Maboto kwa kuwanunulia vifaa vya shule wanafunzi zaidi ya 500

Na Adelinus Banenwa

Zaidi ya shilingi milioni 38 zimetumiwa na mbunge wa Bunda mjini kuwanunulia vifaa vya shule wanafunzi zaidi ya 500 wanaoishi katika mazingira magumu ndani ya Jimbo la Bunda Mjini.

Msaada huu ni sehemu ya juhudi za kuwasaidia watoto hao ili waweze kwenda shule kwa wakati, na umejumuisha viatu, sare za shule, daftari, kalamu, limu paper na begi la shule kwa kila mwanafunzi.

Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi vifaa hivyo, Mhe. Robert Chacha Maboto amesema kama alivyohahidi katika kampeni za uchaguzi wa 2020, kipaumbele chake kama mbunge ni kuwasaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu.

Mhe. Maboto ameeleza kuwa anaguswa sana na watoto wanaoshindwa kwenda shule kutokana na kukosa mahitaji muhimu, kwani yeye mwenyewe amekulia katika mazingira kama hayo.

Amesema kuwa anajivunia kutumia kile kidogo alichojaaliwa ili kusaidia watoto hao kupata elimu.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bunda, Ndugu Abraham Mayaya Magese, alimpongeza Mhe. Maboto kwa juhudi zake kubwa za kuhakikisha anawaletea maendeleo watu wa Bunda.

Mayaya ameeleza kuwa msaada huu ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na akamhimiza Mhe. Maboto kuendelea kutumikia wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini.
Aidha mayaya ametoa pia onyo kwa wale wanaojipitisha, akisisitiza kuwa chama hicho kinaona kila jambo linalofanyika.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Vicent Naano, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alisisitiza kuwa elimu ndiyo njia pekee ya kumuwezesha mtu kufikia malengo yake.

Dkt. Vicent amempongeza Mhe. Maboto kwa jitihada alizozifanya za kuhakikisha watoto wa Bunda wanapata vifaa muhimu vya shule na sasa wanakwenda shule bila kikwazo