UVCCM Bunda yawakumbusha wabunge, madiwani kutoisahau jumuiya hiyo
14 December 2024, 8:39 pm
Kilio kukubwa cha vijana hao ni kutaka ushirikiano kutoka kwa viongozi hao ikiwa ni pamoja na madiwani na wabunge.
Na Adelinus Banenwa
Umoja wa vijana chama cha mapinduzi wilayani Bunda wamewasihi viongozi waliochaguliwa kupitia chama hicho kutoisahau jumuiya hiyo kutokana na majukumu makubwa iliyonayo kwa chama hicho.
Vijana wameyasema hayo katika baraza la kawaida la jumuiya ya Vijana wilaya ya Bunda ambalo limefanyika leo Dec 14, 2024 ambapo pamoja na mambo mengine wamepata nafasi ya kutathmini matokeo ya uchaguzi serikali za mitaa uliofanyika tarehe 27 Nov 2024.
Katika hoja zao vijana hao wamesema mara nyingi wamekuwa wakitumika sana kipindi cha uchaguzi lakini viongozi hao wakishaingia madarakani huisahau jumuiya hiyo ya vijana
Naye mwenyekiti wa jumuiya ya vijana chama cha mapinduzi wilaya ya Bunda Ndugu Muhammad Msafiri amesema umoja wa vijana una imani kubwa na viongozi walipo madarakani kutokana na kazi kubwa anayoifanya mwenyekiti wa CCM taifa na Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania lakini kilio kukubwa cha vijana hao ni kutaka ushirikiano kutoka kwa viongozi hao ikiwa ni pamoja na madiwani na wabunge.
Kwa upande wake Emmanuel Kija ambaye katibu wa Mbunge jimbo la Bunda mjini kwa niaba ya mgeni Rasmi Mhe Robert Chacha Maboto ambaye ndiye Mbunge wa jimbo amewahasa vijana kuzingatia nidhamu pia kutowasema vibaya viongozi waliopo kwa kuwa kufanya hivyo wanakuwa wanakisema vibaya chama ambacho ndicho kilichomuamini kiongozi huyo.
Aidha ndugu kija amewashauri vijana hao kuhakikisha wanamiliki uchumi kutokana na kwamba wao ni nguvu kazi ya chama cha mapinduzi.