Mazingira FM

Bunda DC yafanikiwa kupanda miti elfu 27

24 November 2024, 6:58 pm

Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela akipinda mti kuashiria progaram ya halmashauri ya Bunda DC ya utunzaji wa mazingira

Salumu Mtelela amezielekeza taasisi zote za serikali kuachana na matumizi ya mkaa na kuni badala yake wahakikishe wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na umeme.

Na Adelinus Banenwa

Katika kuendeleza kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi ya kupikia halmashauri ya wilaya ya Bunda leo Nov 24, 2024 imehitimisha kampeni ya upandaji miti takribani elfu 27 katika maeneo mbalimbali ndani ya halmashauri hiyo zikiwemo taasisi za umma na binafsi

Akizungumza katika kilele cha mashindano hayo ya upandaji wa Miti katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela amezielekeza taasisi zote za serikali kuachana na matumizi ya mkaa na kuni badala yake wahakikishe wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo Gesi, umeme n.k

Naye Moshi Amili ambaye ni afisa mazingira halmashauri ya wilaya ya Bunda amesema idara ya mazingira inasisitiza upandaji wa miti na matumizi ya nishati safi ya kupikia badala ya matumizi ya kuni na mkaa ambavyo inachochea kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.

Aidha Amili ameongeza kuwa uwepo wa miti katika maeneo unasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo mafuriko, vipindi vilefu vya jua n.k

Naye Johaness Bucha mratibu wa mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya tabia nchi halmashauri ya wilaya ya Bunda (BCRAP) amesema zoezi la upandaji miti ulilenga upandaji miti kwenye maeneo ya wazi,milia vipara pamoja na maeneo ya taasisi za umma na binafsi lengo kuu likiwa ni kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kutokana na ukosefu wa miti.

Aidha Bucha amesema program hiyo inahusisha pia ufugaji wa nyuki ambapo vikindi mbalimbali ndani ya halmashauri vinapewa elimu kwa lengo la kufuga nyuki na kujipatia kipato.

George Stanley Mbilinyi mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda amesema wao kama halmashauri wanawasisitiza wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni na badala yake wanawapatia elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo Gesi na umeme.

Mbilinyi ameongeza kuwa wanaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa wananchi kutokana na eneo la halmashauri ya wilaya ya Bunda ni vijijini hivyo idadi kubwa ya wananchi wanamatumizi ya kuni hivyo elimu hiyo itakuwa endelevu hasa wakianza na taasisi za umma na binafsi Kama vile shule za msingi na sekondari, makanisa hospitali miongoni mwa taasisi zingine.