Mahafali ya 38 Kisangwa FDC tatizo la maji kubaki historia chuoni
23 November 2024, 3:04 pm
Chuo cha Kisangwa kinatoa kozi za ufundi na ujuzi ambapo mwanafunzi akihitimu lazima awe na uwezo wa kufanya kitu.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa chuo cha Maendeleo ya wananchi Kisangwa (Kisangwa FDC) ameishukuru serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukipatia chuo hicho zana mbalimbali za mafunzo hali inayopelekea wanafunzi hao kujifunza kwa vitendo zaidi.
Edmund Nzowa mkuu wa chuo cha Kisangwa ameyasema hayo kwenye mahafali ya 38 ya chuo hicho yaliyofanyika leo tarehe 22 Nov 2024 ambapo jumla ya wanafunzi 110 kuhitimu mwaka huu.
Nzowa amesema serikali imetoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa majengo na karakana, pia chuo kimechimbiwa kisima cha maji hali iliyotatua kwa kiasi changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.
Mbali na pongezi hizo pia mkuu wa chuo amesema zipo changamoto mbalimbali zinazikikabili chuo hicho ikiwemo upungufu wa mabweni na madarasa, upungufu wa maji safi na salama, upungufu wa wakufunzi miongoni mwa changamoto zingine
Aidha Nzowa amewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao chuoni hapo kwa kuwa kinatoa kozi za ufundi ambazo zinawasaidi katika maisha yao kwa kuajiliwa ama kujiajiri
mkuu huyo wa chuo amesema chuo cha Kisangwa kinatoa kozi za ufundi na ujuzi ambapo mwanafunzi akihitimu lazima awe na uwezo wa kufanya kitu huku akibainisha kozi zitolewazo kuwa ni pamoja an ufundi umeme wa magari, majumbani na viwandani, ufundi ujenzi , ufundi bomba, ufundi uchomeleaji, kilimo na mifugo n.k.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi Mayaya Abraham Magese mwenyekiti wa CCM Bunda, Diwani wa kata ya Mcharo Mhe Samson Sharya amesema anatambua mchango wa chuo cha Maendeleo ya wananchi Kisangwa kwa kuwa wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo wanafanya vizuri sana huko mtaani hasa kupunguza changamoto ya ajira kwa kujiajiri wao wenyewe.