CCM Sazira B wamkataa aliyepitishwa, uchaguzi warudiwa
30 October 2024, 10:11 am
Wanachama wa CCM kata ya Sazira wachachamaa kuhusu mgombea wao kukatwa kisa hajui kusoma na kuandika wamkataa aliyepitishwa na halmashauri kuu ya wilaya.
Na Adelinus Banenwa
Wanachama wa chama cha mapinduzi mtaa wa Sazira B kata ya Sazira wamelazimika kurudia uchaguzi baada kutokukubaliana na uteuzi wa halmashauri kuu ya CCM wilaya kuwapelekea jina la mgombea ambaye hawamkubali.
Wakizungumza na redio Mazingira fm baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura hizo wamedai uchaguzi huo umelazimika kurudiwa kutokana aliyekuwa ameongoza kwa kura kudaiwa kutokujua kusoma na kuandika hivyo halmashauri kuu CCM wilaya kumteua aliyeshika nafasi ya pili hali iliyopelekea mvutano baada ya wanachama hao kutokubaliana na uteuzi huo wakimtaka aliyeongoza.
Kutokana na mvutano huo inadaiwa halmashauri ya CCM ilitoa maelekezo ya kuufuta uchaguzi huo na kuelekeza uchaguzi katika mtaa wa Sazira B kurudiwa ambapo baada ya kurudiwa uchaguzi huo
Zacharia Mwita Malegeli kuibuka mshindi akimzidi kwa kura mpinzani wake Juma Makoye Mahende.
Mkurugenzi wa uchaguzi CCM kata ya Sazira ndugu Kazimoto Kigongo amesema baada ya maelekezo ya halmashauri kuu CCM wilaya wamefanya uchaguzi na tayari zoezi limekamilika.
Mwenyekiti wa CCM kata ya Sazira ndugu Robert Masatu amesema tayari uchaguzi wa marudio umefanyika na mshindi amepatikana hivyo kama chama wameandaa utaratibu mzuri wa kuvunja makundi na kuwasindikiza washindi wote ndani ya kata kwenda kuchukua fomu
Aidha mwenyekiti huyo ametoa rai kwa viongozi kuacha kutengeneza safu zao badala yake waangalie nini hitaji la wananchi ili kupata watu sahihi katika maeneo yao.