Mazingira FM

225 kati ya 380 kuhitimu kidato cha nne Dkt Nchimbi sekondari

11 October 2024, 12:12 pm

Wanafunzi wahitimu shule ya sekondari Dkt Nchimbi, Picha na Adelinus Banenwa

Jumla ya wanafunzi 225 wanatarajia kuhitimu kidato cha nne shule ya sekondari Dkt Nchimbi mwaka huu kati ya wanafunzi 380 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2021.

Kupitia risala yao iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi katika mahafali ya 17 ya shule hiyo, wanafunzi hao wamesema katika kipindi chote cha miaka minne wamefanikiwa katika Nyanja mbali mbali  ikiwemao, taaluma, michezo  nidhamu miongoni mwa mafanikio mengine

Mbali na mafanikio hayo wanafunzi hao wamebainisha changamoto mbalimbali ambazo zimewakabili shuleni hapo ikiwa ni pamoja na utoro wa wanafunzi, baadhi ya wanafunzi wa kike kupata ujauzito, ukosefu wa maabara ya fizikia, upungufu wa walimu, upungufu wa vifaa vya Tehama, pamoja na ukosefu wa jiko la kupikia .

Mgeni rasmi akikabidhi vyeti kwa wahitimu kidato cha nne shule ya sekondari ya Dkt Nchimbi mahafali ya 17, Picha ana Adelinus Banenwa
sauti ya wanafunzi kupitia risala

Kwa upande wake mkuu wa shule ya sekondari Dkt Nchimbi mwalimu Ngassa Mahangila amesema shule hiyo ilianza mwaka 2005 ikiwa na jumla ya wanafunzi 640 na hadi sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1421 ambao wanahudumiwa na walimu 34 kati yao wa kiume 21 na wa kike 13.

Mkuu wa shule ya sekondari Dkt Nchimbi mwalimu Ngassa Mahangila mwenye kipaza sauti, Picha na Adelinus Banenwa

Mwalimu Ngasa amesema mbali na mafanikio mbalimbali waliyoyapata kama shule ikiwemo kufanikiwa kwenye zoezi la wanafunzi kupata chakula shuleni, lakini shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa walimu wa sayansi na sanaa, upungufu wa matundu ya vyoo, upungufu wa vifaa vya kupikia miongoni mwa changamoto zingine.

Sauti ya Mwl Ngassa Mahangila, mkuu wa shule
Diwani wa kata ya Nyasura Magigi Samwel Kiboko mwenye miwani kwa niaba ya mgeni rasmi Mhe Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Robert Chacha Maboto, Picha na Adelinus Banenwa

Naye diwani wa kata ya Nyasura Magigi Samwel Kiboko kwa niaba ya mgeni rasmi Mhe Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Robert Chacha Maboto katika hotuba yake amesema zile changamoto ambazo zimeainishwa kupitia risala ya wanafunzi na taarifa ya shule amezibeba na amehaidi kwamba mbunge atatoa sufuria mbili za kupikia kwa wanafunzi, compyuta tatu huku changamoto zingine zikiendelea kutatuliwa hatua kwa hatua.

Sauti ya Magigi Samwel Kiboko