Mazingira FM

Wakazi wa Zanzibar “wachekelea” maji ya bomba

20 September 2024, 7:08 pm

Diwani kata ya Nyasura Magigi Samwel Kiboko akimtwisha mama ndoo kuashiria uzinduzi wa kituo cha kuchotea maji, Picha na Adelinus Banenwa

Eneo hili liliitwa Zanzibar kutokana na kukosa huduma za muhimu kama vile maji, umeme pamoja na barabara.

Na Adelinus Banenwa

Wakazi wa mtaa wa Zanzibar kata ya Nyasura halmashauri ya mji wa Bunda, wameishukuru serikali kupitia diwani wa kata hiyo, mwenyekiti wa mtaa wa Zanzibar pamoja na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bunda BUWSSA kwa kuwafikishia huduma ya maji safi na salama na kuondokana na adha waliyokuwa wakiipata.

Wakizungumza leo tarehe  20 September 2024 wakati wa kukabidhiwa kituo cha kuchotea maji yaani (DP) wakazi hao wamesema ni muda mrefu wamekuwa wakihangaika na huduma ya maji safi na salama ambapo walikuwa wakilazimika kuchota maji kwenye madimbwi sehemu ambazo hadi wanyama hutumia na wakati mwingine kufuata maji umbali mrefu.

Mwenyekiti mtaa wa Zanzibar Batuli Ndege akimtwisha mama ndoo kuashiria uzinduzi wa kituo cha kuchotea maji, Picha na Adelinus Banenwa

Wakazi wa Zanzibar wameshukuru jitihada za viongozi wao kwa kushirikiana na  BUWSSA ambapo kwa pamoja walishiriki kuchimba mitaro ya mabomba na sasa maji yamepatikana.

Sauti za wakazi wa mtaa wa Zanzibar

Michael Shayo muhandisi kutoka BUWSSA anayeshughulika na matengenezo na uzalishaji, amewapongeza wakazi wa Zanzibar na viongozi wote wa kata ya Nyasura kwa ushirikiano waliouonesha wakati wa utekelezaji wa mradi kwa kuwa walitumia nguvu zao kuchimba mitaro ili mabomba yapite.

Aidha amewataka wakazi hao wa Zanzibar kuhakikisha wanaitunza miundombinu yote ya maji iliyowekwa ili iweze kudumu na pindi watakapobaini mtu yeyote ana nia ya kuhujumu miundombinu hiyo wasisite kutoa taarifa kwa viongozi, pia kwa watumiaji wote wa maji katika kituo hicho wazingatie kulipia bili ili huduma iwe endelevu.

Sauti za Michael Shayo muhandisi kutoka BUWSSA
Diwani kata ya Nyasura Magigi Samwel Kiboko akijaza maji kwenye ndoo kuashiria uzinduzi wa kituo cha kuchotea maji, Picha na Adelinus Banenwa

Naye diwani wa kata ya Nyasura Mhe Magigi Samwel Kiboko amewapongeza wananchi wa Zanzibar  kwa mshikamano waliouonesha katika kipindi chote huku akibainisha kuwa eneo hilo liliitwa Zanzibar kutokana na kukosa huduma za muhimu kama vile maji, umeme pamoja na barabara.

Mhe kiboko amesema kutokana na ushirikianao waliouonesha wakazi hao wa Zanzibar amejitolea kuwalipia bili ya maji kwa wananchi wote waliochota maji kwenye siku ya uzinduzi wa kituo hicho cha maji.

Sauti za diwani wa kata ya Nyasura Mhe Magigi Samwel Kiboko