Mazingira FM

Wanafunzi Dr Nchimbi Sekondari “chakula shuleni kimetufanya tujiamini”

15 August 2024, 9:59 pm

Wanafunzi wa shule ya sekondari Dkt Nchimbi wamesema tangu kuanza kupata chakula shuleni kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana hasa vipindi vya mchana kwa kuwa kabla hawajaanza mpango wa kupata chakula shuleni wanafunzi hao walikuwa wakilala, kuchoka, kundondoka na wengine kutoroka vipindi hivyo vya mchana.

Na Adelinus Banenwa

Wanafunzi wa shule ya sekondari Dr Nchimbi ilyopo kata ya Nyasura halmashauri ya mji wa Bunda wamesema upatikanaji wa chakula shuleni umesaidia kuongeza hali ya kujiamini muda wote wawapo shuleni hadi vipindi vya mchana.

Wanafunzi hao wamesema hayo wakati wakizungumza na Mazingira Fm pembezoni mwa mkutano wa wazazi na walimu uliokuwa ukilenga kujadili maendeleo ya uchangiaji chakula shuleni kwa watoto.

Baadhi ya wanafunzi wamesema tangu kuanza kupata chakula shuleni kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana hasa vipindi vya mchana kwa kuwa kabla hawajaanza mpango wa kupata chakula shuleni wanafunzi hao walikuwa wakilala, kuchoka, kundondoka na wengine kutoroka vipindi hivyo vya mchana.

sauti ya wanafunzi
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliofika shuleni, Picha na Adelinus Banenwa

Kwa upande wao baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliofika shuleni hapo wameipongeza shule hiyo kwa utaratibu mzuri waliouweka wa maandalizi ya chakula kuanzia kwenye usafi hadi utaratibu wa kuhifadhi chakula hicho.

Aidha wamewataka wazazi wengine ambao hawajaanza kutoa mchango wa chakula kwa watoto wao kufanya hivyo kwa kuwa mabadiliko baada ya watoto kuanza kupata chakula shuleni yanaonekana ni mazuri hasa ya kitaaluma.

sauti ya wazazi
Diwani wa kata ya Nyasura Mhe Magigi Samweli Kiboko, Picha na Adelinus Banenwa

Naye diwani wa kata ya Nyasura Mhe Magigi Samweli Kiboko amewapongeza wazazi kwa muitikio waliouonyesha kwenye mchakato huo wa kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni kwa kuwa idadi ya wazazi inazidi kuongezeka kwa wale wanaoleta chakula shuleni ambapo hadi sasa wanafunzi wasiozidi 400 ndiyo waliobaki kati ya wanafunzi 1421 waliopo shuleni hapo.

sauti ya diwani

Mkuu wa shule ya sekondari Dkt Nchimbi mwalimu Benard Ngassa amewapongeza viongozi kuhamasisha suala la chakula shuleni ikiwemo ofisi ya mkuu wa wilaya, ofisi ya mbunge jimbo la Bunda mjini, diwani wa kata ya Nyasura pamoja na ofisi ya  mtendaji wa kata.

Mkuu wa shule ya sekondari Dkt Nchimbi mwalimu Benard Ngassa, Picha na Adelinus Banenwa

Mwalimu Benard pia amewashukuru wazazi kwa muitikio na amesema anaamini kwa wale wazai wachache waliobaki watatoa chakula kwa watoto wao kwa kipindi kifupi kijacho kwa kuwa wanaendelea kuhamasisha wazazi kwa kutumia viongozi wakiwemo wenyeviti wa mitaa na maafisa watendaji ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata chakula shuleni.

sauti ya mkuu wa shule