Mazingira FM

Wananchi Bunda wahamasishwa kutoa maoni dira ya taifa 2025 -2050

13 August 2024, 2:16 pm

Mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto, Picha na Adelinus Banenwa

Kikao cha kujadili na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wa wilaya ya Bunda kuhusiana na dira ya maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2025 hadi 2050.

Na Adelinus Banenwa

Imeelezwa kuwa ili kufikia malengo katika mpango wa dira ya taifa ya miaka 25 ijayo ni lazima kila mtanzania kwa nafasi yake afanye kazi kwa bidii.

Hayo yamesemwa na mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya ya Bunda kilichoketi leo 12 Aug 2024 kujadili vipaumbele vya mpango wa maendeleo wa dira ya taifa 2025 hadi 2050.

Baadhi ya wadau waliofika kwenye kikao cha kamati ya ushauri wilaya ya Bunda

Mhe Maboto amesema ili kuyafikia malengo ya dira ya taifa ni lazima kila mmoja kufanya kazi kwa bidii  pili watu kulipa kodi akibainisha kuwa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 61 watu milioni tano tu ndo wanalipa kodi huku wanaohusika na kilimo ni milioni 8 hali inayofanya jumla ya watu milioni 13 tu wanaofanya kazi ya uzalishaji.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto

Kwa upande wa wadau mwengine waliohudhuria katika kamati hiyo wamebainisha masuala mbalimbali kufanyiwa kazi katika  dira ya Taifa ya maendeleo  kwa mwaka 2025 hadi 2050 katika sekta za Afya, Elimu, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, na Habari na mawasiliano TEHAMA,

Sauti ya wananchi
Mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe Dkt Vicent Anney, Picha na Adelinus Banenwa

Kwa upande wake  mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe Dkt Vicent Anney amewashukuru Wadau wote walioshiriki na  kuchangia katika kutoa maoni yao katika majadiliano hayo. Ambapo amesema ameyachukua maoni yote yaliyotolewa na kuahidi kuyafikisha ili yaweze kufanyiwa kazi na kuwekwa katika mpango wa maendeleo wa  Miaka 25 ijayo.

Sauti ya mkuu wa wilaya Bunda Mhe Dkt Vicent Anney

Baadhi ya Malengo ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 ni pamoja na Kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi Jumuishi unaopunguza umasikini, Kuzalisha ajira na kuchochea mauzo ya Biashara nje ya nchi, Kuongeza na kuimarisha matumizi ya Teknolojia hasa ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Kuongeza uzalishaji wa Viwanda na kuimarisha huduma Bora za Kijamii kwa wote, Kuweka msukumo wa Uongozi tija katika uzalishaji na Uongezaji Thamani sekta za Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Misitu na Madini, Kuongeza ubora wa Elimu na Mafunzo katika ngazi zote.