Wanaume wapigwa marufuku kunyonya maziwa ya wake zao
2 August 2024, 7:32 pm
Ni marufuku wanaume kunyonya maziwa ya wake zao badala yake akina mama watumie maziwa hayo kuwanyonyesha watoto wao.
Na Adelinus Banenwa
Zaidi ya akina mama sabini chini ya mpango wa Compassion wameadhimisha siku ya Unyonyeshaji Mjini Bunda.
Wanawake hao kutoka kanisa la Anglican Tairo na Baptist Nyasura wamesema changamoto kubwa waliyonayo katika unyonyeshaji ni shughuli mbalimbali zinazowakabili pia kutozingatia makusudi maelekezo wanayopewa na wataalam wa afya na lishe.
Pendo Malaki HBI Kituo cha Huduma ya Maendeleo ya kijana na mtoto Baptist Nyasura amesema program hizi zinalenga kuwawezesha watoto kukua katika ustawi unaofaa pia kuwapa elimu akinamama kuwahudumia vizuri watoto wao.
Amesema katika maadhimisho haya ya leo yamesaidia zaidi ya wanawake 70 kupata elimu ya kuwatunza watoto wao na kuzingatia lishe bora na kuepuka changamoto za ukuaji kwa kwa watoto wao.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa halmashauri ya mji wa Bunda Lucy Mwalwayo amesema kuna umuhimu mkubwa kwa mtoto kunyonya maziwa ya mama tangu kuzaliwa mpaka anapofikisha miaka miwili
Lucy amesema katika suala la unyonyeshaji lina pande mbili moja ni mtoto kunyonya maziwa ya mama kipindi cha miezi sita bila kumpa kitu kingine chochote na upande wa pili ni mtoto kunyonya maziwa ya mama kwa kipindi cha hadi anapofikisha miaka miwili na zaidi.
Aidha amesema ni marufuku wanaume kunyonya maziwa ya wake zao badala yake akina mama watumie maziwa hayo kuwanyonyesha watoto wao ili wawe na afya bora.