UWT Bunda wapigwa msasa kuelekea uchaguzi
19 July 2024, 8:28 pm
Wito umetolewa kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025.
Na Adelinus Banenwa
Wito umetolewa kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti ya umoja wa wanawake CCM mkoa wa Mara Bi Nancy Msafiri Sesani alipokutana na wanawake wa UWT takribani 1030 wilayani Bunda kuzungumza nao kuelekea uchaguzi serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Katika kongamano hilo mwenyekiti Nancy aliambatana na katibu wa UWT mkoa wa Mara, mjumbe wa baraza la wanawake UWT taifa na mkurugenzi wa kituo cha nyumba salama Bi Rhobi Samweli, Latifa Hamis mjumbe wa kamati ya utelelezaji mkoa wa Mara, miongoni mwa viongozi wengine.,
Bi Nancy amesema kutokana na wanawake kuwa wengi inaweza kusaidia kushika nafasi mbalimbali endapo mwanamke akigombea na kuungwamkono na wanawake wenzake.
Naye Latifa Hamis ambaye ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji mkoa amesema ili mwanamke aweze kupata nafasi ya kuruhusiwa na mume wake kushiriki katika kugombea nafasi za uongozi inatakiwa waache ukatili kwa waume zao.
Amesema mbali na ukatili unaofanywa na wanaume kwa akina mama na watoto lakini pia wanawake wamekuwa wakifanya ukatili dhidi ya waume zao ikiwa ni pamoja na kuwanyima unyumba hali inayopelekea wanaume kuwazuia wanawake hao kushiriki kwenye uchaguzi na kupiga kura.
Kwa upande wake Rhobi Samweli amesema zipo changamoto mbalimbali watakazokutana nazo wanawake pale watakapochukua hatua ya kugombea ikiwemo ukatili wa kisiasa lakini hawapaswi kukata tama badala yake aina yoyote ya ukatili watakayokumbana nayo hawana budi kutoa taarifa kwa viongozi wao ili waweze kuishughulikia.
Naye mwenyekiti wa UWT wilaya ya bunda Maryciana Sabuni amewataka wanawake kuwa na umoja na ujasiri kuelekea uchaguzi pia wasisite kugombea kwa kuwa akina mama ni jeshi kubwa.