Ndama kutetea nafasi yake kwenye uchaguzi
7 July 2024, 5:56 pm
“Niko tayari kutetea nafasi yangu kwa kuwa kazi nilizozifanya ndani ya kipindi cha miaka mitano zinaonekana“
Na Adelinus Banenwa
Mwenyekiti wa Idara ya maji kata ya Bunda stoo halmashauri ya mji wa Bunda Ndugu Mtaki Bwire Ndama amesema atatetea nafasi yake ya uwenyekiti kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.
Akizungumza na kipindi cha siasa na maendeleo kinachorushwa na radio Mazingira FM Ndugu Mtaki amesema yapo mengi yanayomfanya aitetee nafasi yake hasa yale aliyoyafanikisha katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake kama mwenyekiti wa mtaa.
Mtaki amesema katika kipindi chake cha uongozi, miongoni mwa mambo aliyoyafanikisha ni pamoja na Upimaji wa viwanja vya wananchi karibia asilimia 85 ya mtaa, Upatikanaji wa eneo la kujenga hospitali ya halmashauri ya mji wa Bunda ambapo aliwashawishi wananchi kujitolea maeneo yao, Upatikanaji wa shule mpya ya msingi ambayo imesaidia wanafunzi kutotembea umbali mrefu ambayo ilikuwa adha kubwa hasa kipindi cha mvua.
Sambamba na hayo pia amesema katika kipindi hichohicho amefanikisha kupatikana kwa eneo la ujenzi wa shule ya sekondari ya Bunda stoo ambapo wananchi walijitolea maeneo yao, pia amefanikisha upatikanaji wa eneo la soko katika mtaa wake ambapo amesema maeneo hayo yote yamepatikana kutoka kwa wananchi baada ya juhudi zake kwa kushirikiana na viongozi wengine akiwepo diwani wa kata hiyo, viongozi wa halmashauri pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya.
Aidha ndugu Mtaki ameongeza kuwa changamoto kubwa kwa sasa katika mtaa wake ni suala la ubovu wa barabara na kumalizia asilimia 25 ya wananchi ambao hawajapimiwa viwanja vyao, huku akitaja yapo makundi mbalimbali ya watu wenye nia ovu wanaotoa taarifa za uongo kuhusu zoezi la upimaji wa viwanja lakini anashukuru kwa kuwa jambo hilo linafanyika kwa uwazi na wananchi wanaelewa.
Bwire amesisitiza kuwa yupo tayari kutetea nafasi yake kwa kuwa kazi alizozifanya zinaonekana kwa macho na wakazi wa mtaa wa Idara ya maji wanaziona.