Mazingira FM

Waganga tiba asili Bunda walaani mauaji ya watu wenye ualbino

3 July 2024, 12:38 pm

Mwenyekiti wa chama cha waganga wa tiba asili na tiba mbadala Bunda Naggo Tungalaza, Picha na Adelinus Banenwa

Waganga wa tiba asili na tiba mbadala Bunda wamelaani mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na mauaji mengine yenye imani za kishirikina, wakisema wanaofanya hivyo siyo waganga wa tiba asili bali ni waganga wa kienyeji.

Na Adelinus Banenwa

Chama cha waganga wa tiba asili na tiba mbadala wilaya ya Bunda kimetoa tamko la kulaani mauaji ya watu wenye ualbino na matukio mengine kama hayo.

Tamko hilo limetolewa na mwenyekiti wa chama hicho wilayani Bunda ndugu Naggo Tungalaza kwenye mkutano uliowakutanisha waganga wote wa tiba asili na tiba mbadala wilaya ya Bunda uliolenga kuwakumbusha majukumu yao kwa mujibu wa sheria namba 23 ya mwaka 2002.

Baadhi ya wanganga wa tiba asili wilayani Bunda, Picha na Adelinus Banenwa

Tungalaza amesema wao kama waganga wanalaani kitendo kilichotokea mkoani Kagera wilaya ya Muleba cha mtoto mdogo kuuawa huku mganga akitajwa kuhusika katika tukio hilo, ila wao wanaamini mganga mwenye kufuata misingi ya kiapo chake hawezi kufanya matukio ya ramli chonganishi wala mauaji.

Sauti ya Naggo Tungalaza
Jacob Sira Matiko mjumbe wa kamati ya maadili baraza la tiba asili na tiba mbadala Tanzania, Picha na Adelinus Banenwa

Kwa upande wake Jacob Sira Matiko mjumbe wa kamati ya maadili baraza la tiba asili na tiba mbadala Tanzania amewakumbusha waganga wote wa tiba asili majukumu yao hasa kuzingatia misingi ya sheria kama ilivyoainishwa kwenye sheria yao ya mwaka 2002.

Amesema katika sheria hiyo namba 23 ya mwaka 2002 haimtambui mganga wa kienyeji bali mganga wa tiba asili.

Sauti ya Jacob Sira
Stephano Machage kutoka ofisi ya mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Bunda Picha na Adelinus Banenwa

Naye Stephano Machage kutoka ofisi ya mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Bunda ambao ndiyo wenye dhamana ya kufuatilia usajili wa waganga hao amesema matatizo mengi yanasababishwa na waganga kutokana na kutofuata misingi ya kazi zao hasa kutosajili shughuli zao, kufanya ramli chonganishi na utabili.

Stephano amewaonya waganga wanaofanya kazi zao ndani ya Bunda bila vibali na wale wanaokiuka taratibu za kazi zao kuwa ofisi ya mganga mkuu wa halamshauri ya mji wa Bunda haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

Sauti ya Stephano Machage