Mtambi: Watumishi timizeni wajibu wenu, shule ya mwisho kupewa kinyago
27 June 2024, 12:22 pm
Kanal Mtambi amewataka watumishi kuzingatia maadili ya taaluma zao huku akitoa maelekezo ya marufuku shule kupata sifuri matokeo ya kidato cha nne mkoa wa Mara.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa mkoa wa Mara Mhe Kanal Evans Mtambi amewataka watumishi kuzingatia wajibu wao kwa mujibu wa taaluma zao katika kuwatumikia wananchi.
Kanal Mtambi amesema hayo katika kikao na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara kilichofanyika leo Juni 26, 2024 katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Katika kikao hicho RC Kanal Mtambi amesisitiza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na elimu, afya, matumizi ya vyoo kwa wananchi miongoni mwa mambo mengine.
Katika sekta ya elimu Mhe Kanal Mtambi amesema Bunda haifanyi vizuri kwenye sekta ya elimu huku akitaja asilimia 69 ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wanapata division 4 na 0.
Mtambi amesema ndani ya mkoa wa Mara hataki shule yoyote wanafunzi wake kupata alama sifuri kwenye matokeo ya kidato cha nne.
Katika sekta hiyo ya elimu mkuu wa mkoa ameelekeza kuwa wilaya inatakiwa kutengeneza ngao ambayo itapewa shule itakayofanya vizuri kwenye halmashauri ili kuleta chachu, huku kwa shule itakayokuwa ya mwisho kwa Halmashauri, kutengenezewa kinyago kitakachokuwa kikikaa kwenye ofisi ya mkuu wa shule ambapo lengo likiwa ni hilohilo la kuongeza chachu ya kufanya vizuri kwenye masomo.