Raymond: Wafanyabiashara tumieni benki kwa usalama wa fedha
17 June 2024, 7:01 pm
“Wafanyabiashara msipende kutunza pesa zenu majumbani kuna hatari nyingi mfano moto, wezi n.k pelekeni benki fedha zitakuwa salama”, Raymond.
Na Adelinus Banenwa
Baadhi ya wafanyabiashara mkoani Mara wamelalamikia uwepo wa makato makubwa kwenye taasisi za kifedha hasa mabenki hali inayopelekea baadhi yao kuamua kutokutunza fedha zao kwenye taasisi hizo.
Madai hayo yametolewa mjini Musoma na wafanyabiashara hao kwenye kongamano la klabu ya wafanyabiashara wa NMB ambapo wameziomba mamlaka husika kungalia namna ya kupunguza makato hayo.
Katibu wa Chama Cha Wafugaji Wilaya ya Butiama, Peter Machugu amezitaka taasisi za fedha kukaa na serikali kuangalia namna ambavyo makato haya yanaweza yakashuka ili kuwapa nafuu wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla.
Amesema kuwa kutokana na hali hiyo wamejikuta wakifanya biashara katika mazingira hatarishi kutokana na kulazimika kutembea na fedha kwenda minadani kwaajili ya kununua mifugo.
Meneja Mwandamizi, Kitengo cha Biashara kutoka NMB Makao Makuu, Reynold Tony amesema hali ya uwekaji wa amana kwenye taasisi za kifedha nchini bado ipo chini na kwamba kutokana na hali hiyo benki yake imekuwa ikibuni huduma mbalimbali ambazo ni rafiki ili kuhakikisha wafanyabiashara wengi wanatumia mfumo huo.
Raymond amesema wamebaini wapo wafanyabiashara wengi ambao hawatumii mifumo ya kibenki jambo ambalo siyo salama kwani utunzaji wa fedha ndani una hatari nyingi ikwemo fedha kuibiwa, kuungua moto na mambo mengine.