Mazingira FM

Mtoto atupwa saa chache baada ya kuzaliwa, wasamalia wamuokota

14 June 2024, 6:44 pm

Kitandani ni mtoto aliyeokotwa, pamoja nesi aliyempokea mtoto huyo na kuanza kumpatia huduma, Picha na Adelinus Banenwa

Mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na masaa kadhaa tangu kuzaliwa ameokotwa baada ya kutupwa na mama yake punde tu baada ya kujifungua.

Na Adelinus Banenwa

Mtoto huyo jinsia ya kike ameokotwa leo June 14 mtaa wa Mapinduzi kata ya Bunda mjini  wilayani Bunda na wapitanjia baada ya moja ya waokota makopo ya maji yaliyotumika kumkuta mtoto huyo akiwa amewekwa kwenye mfuko mbadala na kutupwa kwenye majani.

Magige Machumu mjumbe wa serikali ya mtaa amesema taarifa ya mtoto kutupwa aliipata majira ya  asubuhi ya saa moja na muokota makopo anayefahamika kwa jina maarufu Maringosaba na alipofika eneo la tukio alikuta watu tayari wamekusanyika ndipo alipompigia mwenyekiti wa mtaa simu ili afike kuona tukio hilo.

Sauti ya machumu mjumbe serikali ya mtaa wa Mapinduzi

Naye mwenyekiti wa mtaa wa Mapinduzi Ndugu Daniel David Yapanda amesema majira ya saa mbili asubuhi akiwa ofisi za NIDA alipokea simu kutoka kwa moja ya wajumbe wa serikali ya mtaa kumjulisha kuhusu tukio la mtoto kutupwa na alipofika eneo la tukio alikuta tayari mtoto amepelekwa kituo cha afya cha Bunda.

madaktari wakiendelea kumpatia huduma mtoto ili awe salama, Picha na Adelinus Banenwa

Yapanda amesema alifika kituo cha afya alikuta tayari mtoto huyo ameanza kupewa huduma hivyo alichukua jukumu la kumpigia afisa mtendaji wa kata pamoja na jeshi la polisi kwa lengo la kuwapa taarifa kwa kuwa hadi wakati huo mama aliyetupa mtoto alikuwa hawamfahamu.

Sauti ya Daniel yapanda

Royce Erenest ambaye ni nesi kituo cha afya Bunda anasema wakati anapita eneo la tukio alisikia watu wanasema mtoto ametupwa na baada ya kufika ni kweli alikuta mtoto kafungwa kwenye mfuko huku baadhi ya wananchi wakizua asitolewe hadi waite jeshi la polisi,

Bi Royce anasema alichukua jukumu la kuwashawishi watu wale ili wambebe mtoto huyo kumpeleka hospitali kwa kuwa aliamini kuzidi kuchelewa kungepelekea mtoto huyo kupata madhara ya kiafya.

Mtoto baada ya kupewa huduma na madaktari wa kituo cha afya Bunda, Picha na Adelinus Banenwa

Bi Royce ameongeza kuwa wananchi walimuelewa na alipofika kituo cha afya mtoto alipimwa uzito na wingi wa oksijeni pia hali ya joto pamoja na kipimo cha vvu ambapo waligundua vipimo vingine vipo sawa isipokuwa alikuwa na baridi kali hivyo wao kama wahudumu wa afya alimpatia huduma ya joto kwa kuwa vifaa wanavyo.

Sauti ya Royce Erenest

Mtendaji wa kata ya Bunda mjini bi Kagoye Mwenge amesema ni tukio la kusikitisha kuona mama aliyebeba mimba miezi tisa alafu anamtupa mtoto wake wa kumzaa ni kitendo cha ukatili na ni cha kulaaniwa.

Aidha amewataka wananchi kufahama kuwa yako matukio ya kumsubili polisi na matukio ya kuchukua hatua mapema.

Bi Kagoye amesema tukio lolote ambalo linamuhitaji mtu kwenda hospitali kwa ajili ya kunusuru maisha yake ni vema wananchi wakawa na uharaka wa kufanya hivyo lakini ikiwa tukio limeshatokea kama vile mauaji iwe ya kujiua au kuuliwa hayo ni vema likasubiliwa jeshi la polisi au maelekezo kutoka kwa viongozi wengine.

Aidha Bi Kagoye amesema wanamshukuru mungu mtoto anaendelea vizuri na wao kama serikali ya kata wataendelea kushirikiana na jeshi la polisi na ofisi ya ustawi kujua hatma ya mtoto huyo na kumtafuta mama aliyetenda tukio hilo.

Sauti ya Kagoye Mwenge