Wawili jela miaka 30 kwa unyang’anyi wa kutumia silaha
8 June 2024, 5:39 pm
inadaiwa washtakiwa walimvamia Minza Kongo kisha kumkata mapanga na kuchukua vitu mbalimbali ikiwepo radio aina ya Subwoofer na pesa taslimu tshs 230,000/.
Na Adelinus Banenwa
Mahakama ya wilya ya Butiama imewahukumu watu wawili kwenda jela miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama ya wilaya ya Butiama Mh. Judith Semkiwa ambapo waliohukumiwa ni Giraguru Kitati na Mwita Juma kwa unyang’anyi kwa kutumia silaha chini ya kifungu cha 287 A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo 2022.
Awali Mwendesha Mashtaka kiongozi wa serikali wakili Gaston Gallus Kayombo wa wilaya ya Butiama akiwasomea maelezo ya awali ameeleza kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo mnamo tarehe 17 mwezi April mwaka 2023 huko kijiji cha Kisamwene kilichopo wilaya ya Butiama ambapo washtakiwa wote wawili wakiwa na mwenzao mmoja ambaye hakukamatwa walimvamia Minza Kongo kisha kumkata mapanga na kuchukua vitu mbalimbali ikiwepo radio aina ya Subwoofer na pesa taslimu tshs 230,000/.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka Kiongozi Gaston Gallus Kayombo akisaidiwa na Mwendesha Mashtaka Joachim Butahe walikuwa na mashahidi 6 ili kuthibitisha kesi ya Jamhuri, huku upande wa utetezi walikuwa na mashahidi wanne.
Mheshimiwa Judith Semkiwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Butiama akisoma hukumu hiyo alieleza kuwa upande wa Jamhuri umethibitisha kesi yake pasipo na kuacha shaka lolote na hivyo kuwatia hatiani washtakiwa kwa kosa wanaloshtakiwa nalo la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Washtakiwa hao walipoulizwa kama wanajambo lolote la kusema ili wapunguziwe adhabu walijibu hawana jambo lolote la kusema, huku Mwendesha Mashtaka Gaston Kayombo akiomba adhabu kali itolewe kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwao na kwa wengine wenye nia ya kutenda vitendo hivyo.