Waathirika wa mafuriko Lamadi wapongeza viongozi kuwatembelea
7 May 2024, 2:40 pm
Na Edward Lucas
Wahanga wa mafuriko kata ya Lamadi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu wamewashukuru viongozi wa CCM mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Busega kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao.
Wakizungumza na Radio Mazingira Fm kwa nyakati tofauti baada ya kutembelewa na viongozi hao wamesema imewapa matumaini makubwa ya changamoto zao kushughulikiwa na kuwasisitiza viongozi kusimamia vizuri misaada yote itakayotolewa ili iwafikie walengwa.
Viongozi waliowatembelea wananchi hao kwa siku ya jana tarehe 6 May 2024 ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed na Mkuu wa Wilaya ya Busega Faidha Salum akiwa na viongozi wengine wa halmashauri ya Busega.
Akizungumzia ziara hiyo Diwani wa kata ya Lamadi, Bija Laurent Bija amesema jumla ya kaya 413 zimeathirika na mafuriko hayo na kuwafanya wananchi kukosa makazi na chakula na kwamba viongozi waliofika wameahidi kutoa mahitaji ya chakula na malazi ili kusaidia katika changamoto inayowakumba.