Pikipiki za CCM Bunda zazua kizaazaa, viongozi watoa matamko
1 May 2024, 10:45 am
Wengine watajwa kuzitumia kama bodaboda wengine kubebea samaki wengine watajwa kuzigawa kwa watoto wao
Na Adelinus Banenwa
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi CCM wilaya Bunda wakili Leonard Magwayega amepiga marufuku kwa viongozi wa jumuiya hiyo waliopewa pikipiki za chama kuzitumia kinyume na maelekezo ya chama.
Wakili Magwayega amesema hayo kwenye maadhimisho ya wiki ya wazazi ambapo kiwilaya yamefanyika kata ya Nyasura mjini Bunda April 30, 2024.
Magwayega amesema pikipiki zilizotolewa na mwenyekiti CCM taifa zilitolewa kwa lengo la kuimarisha uhai wa chama lakini kwa sasa pikipiki hizo zimeshuhudiwa zikifanya shughuli binafsi badala ya kufanya shughuli za chama
Magwayega amesema kuna pikipiki zimeshuhudi zikibeba abiria, samaki na mizigo mikubwa zaidi ya uwezo wa pikpiki zenyewe
Magwayega amemuelekeza katibu wa jumuiya hiyo wilaya ya Bunda kuwanyang’anya pikipiki hizo viongozi wote wa jumuiya watakaobainika wanakwenda kinyume na maelekezo ya chama.
Naye katibu wa siasa na uenezi CCM wilaya ya Bunda Ndug. Gasper Petro Charles amesema tayari yapo malalamiko mengi juu matumizi ya pikipiki hizo
Aidha Gasper amesema hadi sasa wameshawanyang’anya viongozi kadhaa pikipiki na kuzilejesha wilayani kutokana na kwenda kinyume na maelekezo ya matumizi yake.